Vielezi

- Kielezi ni neno litumikalo kuonyeshea jinsi tendo linavyofanyika

- Kielezi aidha huonyeshea sababu ya kitendo kufanyika au wakati wa kutokea kwa vitendo. Aidha, huonyeshea mahali kitendo kilipotendeka.

Mifano: kasi, polepole, haraka, sana, vizuri, juu, chini, mapema, kivivu n.k.

Kielezi kinaweza kueleza:

  • Hali ya kitendo; yaani jinsi kitendo kilivyofanyika (vipi) k.m. Anatembea haraka.
  • Wakati wa kutukia kwa kitendo (lini) k.m. Aliondoka a s u b u h i. Nitaondoka mwakani.
  •  Mara ngapi kitendo kimetokea. k.m. Tulionana mara nyingi. iv. Mahali: Kitendo kilitokea wapi? k.m. Ndege alipaa angani.

Ni muhimu kuelewa kuwa, yapo maneno kadhaa ambayo hutumika kama vielezi na pia kama visifa. Nayo ni: vyema, vizuri, vibaya, kidogo, vikali n.k.

Zitazame sentensi zifuatazo:

  • Anasoma vyema. ( kielezi)
  • Vitabu hivi ni vyema. ( kisifa)
  • Nitilie maji kidogo. ( kisifa)
  • Aliongea kidogo. ( kielezi)

Aina mbalimbali za vielezi

Vielezi vya idadi

Vinajulisha kuwa kitendo kimetoka mara ngapi au kiasi gani.Vielezi vya idadi hasa hujibu maswali:kiasi gani? au mara ngapi?

Mifano

Tuonge mara ngapi kwa siku - Tuonge mara kadhaa kwa siku

Atakunywa uji kiasi gani? - Atakunywa uji kiasi kidogo tu.

Yeye huja hapa kila mara. Yeye huja hapa siku zote. Yeye huja hapa daima. 

 

Vielezi vya mahali (wapi)

Hutumika hasa kuonyesha mahali ambapo kitendo kimetendeka . Aghalabu hujibu swali:"wapi?"

Mifano

Mti ulianguka wapi? - Ulianguka majini

Mvuta bangi atafungwa wapi - atafungwa gerezani

Aliumia kichwani.

Tunalima shambani.

Wanasomea sebuleni.

 

Vielezi vya hali/jinsi/namna

Vinaeleza  jinsi au namna kitendo kinavyotendeka. Hutumika kijibu swali: (vipi?)

ghafla, polepole, kijinga, kizungu, kivivu, kisasa, kimoyomoyo, kimyakimya, vibaya, vyema,

Mifano

Utasoma vipi? - Nitasoma kimoyomoyo

Amecheka namna gani? - Amecheka vizuri

 

Vielezi vya wakati (lini)

Vinaonyesha wakatii wa kutokea kwa kitendo. Aghalabu vielezi hivi hujibu swali:lini?

Mifano

Lucia atarudi lini? - Atarudi alasiri.

Mahu aliondoka wakati gani?  - Aliondoka adhuhuri.

Ataondoka mwezi ujao. Ataondoka kesho kutwa. Ataondoka punde tu.

 

Zoezi

1. Mtoto alianguka akaumia _____ . (mbaya)

2. Alifanya kazi _____ (upole) akachelewa kuimaliza.

3. Mahindi yamevunwa _____ (nyingi) mwaka huu.

4. Tulienda mjini ____ (miguu) bila gari.

5. Moraa ameumia _____ (ndogo) alipoanguka.

6. Mei amesoma _____  (moyo) mpaka mwisho.

7. Wageni wamefika ______ (nyumba) jioni.

8. Bi arusi amevalia ____ ( njema).

 

Vielezi vya mkazo

Hivi ni vielezi takriri. Hutumiwa kutilia mkazo au kusisitizia jambo linalizungumziwa. Vielezi hivyo ni kama vifuatavyo:

1. kutwa kucha

2. Uso kwa macho

3. hakiri habari

5. hali na mali

 

Matumizi katika sentensi

1. Tangu Zuma apigwe kalamu, sasa hana kazi wala bazi.

2. Babu zetu wameishi hapa miaka nenda kiaka rudi.

3. Matamba hataki kunilipa pesa alizokopa kwangu, kila nikimdai, ananitilia huku akinitolea kule.

4. Tuliishangilia tuzo aliyopewa Pro. Wangari Maathai kwa shangwe na hoihoi.

 

Zoezi

Jaza nafasi zilizo wazi kwa vielezi vya mkazo kamilifu.

1. Mauzauza anachungulia kaburi, si hayati si ______.

2. Usikate mti wowote popote bure ______.

3. Watoto wasikubali kuajiriwa, waendelee kusoma daima _____.

4. Wanaokata miti ovyo tuwaonye na tuwakemee dhahiri ______.

5. Dawa za kulevya ni hatari, sitazitumia liwalo na _____.