Insha ya hotuba

 

- Katika insha ya hotuba, mwandishi anatakikana kuyanukuu maneno ya mtoa hotuba moja kwa moja.

- Usemi wa kauli halisi hutumika katika kuandikia insha ya hotuba.

 

Zingatia yafuatayo kuhusu insha ya hotuba.

  • Kichwa: Je utachaguaje kichwa cha insha yako? Utahitajika kuongozwa na suala ambalo mtoa hotuba analitilia mkazo zaidi katika hotuba yake.
  • Utangulizi: Utaonyesha jinsi mtoa hotuba alivyofika jukwaani (hili hutegemea muundo wa swali). Pili, katika utangulizi mtoa hotuba atawasalimia na kisha ajitambulishe kwa wale wanaomsikiliza. Kulingana na muundo wa swali, insha yako inaweza kuwa na tangulizi mbili. 
  • Mwili: Sehemu hii ndiyo nguzo ya hotuba. Katika sehemu hii, maudhui yatategemea mada (mambo) yatakayozungumziwa katika hotuba Maudhui hayo hutegemea: i) ni nani anayetoa hotuba na ii) ni akina nani wanaomsikiliza. Kwa hivyo, uandikapo insha ya hotuba, lazima ujiulize maswali yafuatayo kabla ya kuandika insha yako. - Ni nani anayetoa hotuba? - Ni watu wapi wanaomsikiliza? - Ni yapi anayostahili kuwaeleza? - Ni yapi matakwa au mahitaji ya wanaomsikiliza?
  • Tamati: Katika sehemu hii, anayetoa hotuba hutamatisha hotuba yake. Huwashukuru watu kwa kumsikiliza. Huwapa changamoto au himizo fulani. Kwa mfano, kuchanga pesa kwa kujitolea iwapo ametoa hotuba katika mkutano wa kuchanga pesa, kuhifadhi mazingira n.k. Kisha mwandishi wa insha ataeleza jinsi mtoa hotuba alivyotoka jukwaani na vile vile aeleze hisia za waliomsikiliza k.m. “Kisha mgeni mheshimiwa alitoka jukwaani na kuelekea kitini huku umma ukimshangilia.”

 

Mfano:

Wewe ni mbunge. Toa hotuba ya kumkaribisha waziri wa serikali huku ukimweleza matatizo yanayowakabili watu wa eneo lako.

Kichwa: k.m. ZINDUKO LA MWOGA NI UKEMI.

Utangulizi - Kumkaribisha waziri na kumpongeza kwa kuwatembelea

Mwili: – Matatizo ya usalama katika eneo lako. Ombi la kujengewa kituo cha polisi - Matatizo ya huduma za matibabu – ombi la kujengewa zahanati. - Ubovu wa barabara – ukulima na biashara zimeathirika - ombi la kukarabatiwa barabara. -  Elimu – uhaba wa shule na walimu - Ombi la kujengewa shule na kuletewa walimu. - Uhaba wa vifaa vya kufundishia - Ombi la kusaidiwa na wizara ya elimu. - Tatizo la pombe haramu na dawa za kulevya – kuomba serikali iwachukulie wahusika hatua  kali, hasa wauzaji wa pombe na dawa hizo. -

Ukosefu wa maji safi - Pendekezo la kuchimbiwa kisima na serikali.

Tamati: Kumkaribisha waziri ili awahutubie waliofika.

 

1. Andika hotuba ya afisa wa elimu inayoanza: "Bwana mwenyekiti, Mwalimu Mkuu, wazazi,walimu na wanafunzi ...’’

2. Andika hotuba ya:

  • Chifu kwa wanakijiji wake.
  •  Mwalimu Mkuu katika sherehe za kutoa zawadi shuleni.
  •  Mbunge wa eneo lako wakati wa mkutano wa kuchangiza pesa shuleni mwenu.
  •  Afisa wa Afya kwa wanakijiji kuhusu usafi wa mazingira