Insha ya methali

- Katika swali la sampuli hii, mtahini anaweza kutoa methali na kumtaka mtahiniwa aandike insha kuhusu mada hiyo.

- Vilevile mtahini anaweza kutoa methali ikiwa sentensi ya kutamatisha

 

Mifano ya kuuliza swali kuhusu methali ni kama:

  • Andika insha ya kichwa kifuatacho; MCHUMIA JUANI HULIA KIVULINI
  • Itamatishe insha yako hivi: ... Tangu siku hiyo nilielewa kuwa, yote yang’aayo si dhahabu. Au ... kweli wahenga hawakukosea walipo nena wema hauozi. Ni muhimu kung’amua kuwa maswali haya matatu yanatahini kuhusu methali ingawa kwa njia tofauti.

 

Mambo ya kuzingatia:

1. Elewa methali inayozungumziwa uweze kuieleza na hata kujua methali badala yaani methali nyingine yenye maana na matumizi sawa na hiyo.

2. Tunga kisa ambacho kinaonyesha ukweli wa methali hiyo.

3. Hatimaye ni lazima uelewe funzo linalopatikana katika methali hiyo. Kwa hivyo, unapoandika insha yako, sharti iwe na sehemu zifuatazo:

  • Kichwa
  • Utangulizi: Eleza maana na matumizi ya methali. Vilevile, taja methali (iwapo ipo) nyingine iliyo na maana na matumizi sawa na methali unayoeleza kuhusu.
  • Mwili : Tunga kisa ambacho kitaonyesha ukweli wa methali hiyo. Lazima utunge kisa chako wala usinakili labda hadithi uliyosoma kitabuni au labda kusimuliwa.
  • Tamati: Katika sehemu hii, utaeleza funzo ambalo linapatikana kutokana na methali hiyo. Funzo linaweza kuwa ni onyo (tusifanye jambo fulani), kutuhimiza tutende wema, kutia moyo n.k.

 

Kwa kifupi, lazima uzingatie yafuatayo:

  1. Ni nini maana ya methali hii?
  2. Je, methali hii ina maana sawa na methali ipi au zipi nyingine?
  3. Je, ni yapi niliyoshuhudia hadi nikaamini kuwa ukweli wa methali hiyo k.m.mvumilivu hula mbivu?
  4. Ni funzo lipi tupatalo kutokana na methali hii?

 

Zoezi

Andika insha zinazoisha:

1. ... Tangu siku hiyo niliamini kuwa yote yang’aayo si dhahabu.

2. .... kweli kupotea njia ndilo kujua njia.

3. ... nami nikaamini kuwa mcha mwana kulia hulia mwenyewe.

4. ... wahenga hawakukosea waliposema mchimba kisima huingia mwenyewe.

5. ... mama alibaki mdomo wazi huku akituambia kila ndege huruka na mabawa yake