Barua ya kirafiki

- Barua ya kirafiki pia huitwa barua ya kidugu.

- Barua ya kirafiki huandikwa kwa rafiki au hata kwa mtu wa familia.

- Unaweza kumwandikia rafiki au ndugu ukimweleza mambo mengi k.m kumjulia hali, kumpongeza, kumpa pole, kumwalika katika sherehe n.k..

Katika barua ya aina hii, zipo sehemu sita;

1. Anwani ya mwandishi.

- Anwani huandikwa katika sehemu ya juu ya karatasi upande wa kulia.

- Katika kuandika anwani, yafuatayo hujumulishwa:

  • Makao ya mwandishi k.m. Shule yake, kijiji chake, mtaa wake n.k;
  • S.L.P. (Sanduku la posta); Nambari ya sanduku la posta apokeapo barua;
  • Mji ambapo posta apokeleapo barua zake ipo;
  • Tarehe aandikapo barua hiyo; Tarehe, mwezi na mwaka.

 

2. Mkusudiwa.

- Sehemu hii huonyesha ni nani anayeandikiwa barua k.m. Kwa mpendwa mama/ kaka/ shangazi/mwanangu n.k.

 

3. Aya ya kwanza au utangulizi wa barua yako.

- Katika utangulizi yafuatayo huorodheshwa:

  • Maamkizi - Kujuliana hali.
  • Pongezi, labda kwa barua ya hapo awali.
  • Msamaha labda kwa kuchelewa kujibu barua n.k.

 

4. Kiwiliwili

- Sehemu hii huchukua nafasi kubwa katika barua ya kirafiki.

- Katika sehemu hi, mtahiniwa au mwandishi wa barua, hueleza mambo kadhaa kulingana na swali.

 

5. Aya ya mwisho/Tamati. 

- Katika aya hii, mwandishi hutoa salamu kwa watu kadhaa; yaani, hutaka watu hao kufikishiwa salamu zake/humwomba aliyemwandikia kumjibu/huwasilisha jambo lolote.

- Ni vizuri ujumbe kama huo kuongezewa uzito kwa methali murwa k.m. - Ndugu soma kwa bidii kwani elimu ni nguzo aushini; au, jiepushe na anasa kwani mchezea tope huchafuka. n.k.

 

6. Wasalaam

- Sehemu hii huwa inaonyesha aliyeiandika barua hiyo.

- Sehemu hii hufuata tu pindi baada ya aya ya tamati.

- Huandikwa kulingana na uhusiano wa mwandishi na mwandikiwa wa barua k.m. dada/kaka yako wa toka nitoke, msena wako wa kufa kuzikana, mwanao wa pekee, mama yako mpendwa n.k.

- Mbali na kuelewa vipengele hivyo vya barua ya kirafiki ni jambo la umuhimu mtahiniwa kuelewa anayotakiwa kuandika katika waraka wake.

Maudhui ya barua

- Yale atakayoandika hutegemea jinsi swali lilivyo. Hebu upigie darubini mfano huu:

Mwandikie barua ndugu yako aliye mbali umweleze hali ya mambo nyumbani.

Katika swali la aina hii, kabla hujaanza kulijibu, lazima utilie maanani yafuatayo.

  • Je nduguyo yuko wapi?
  • Nduguyo alitoka kiamboni lini?
  • Tangu atoke nyumbani yapi ambayo yametendeka nyumbani / kijijini au mtaani / kwa watu wa aila kama vile shangazi na hata kwa marafiki zake nduguyo? Mweleze hayo yote
  • Unaweza kuanza kumweleza mambo mazuri kisha iwapo kunayo mabaya yametendeka, pia mjulishe ili aelewe hali halisi ya mambo nyumbani.

 

Mfano wa barua

 

Shule ya Wamahiga, 

S.L.P 17, 

SABASABA.

20-02-2006.

 

Kwa baba mpendwa,

Zipokee salamu tele kutoka kwangu. Mimi ni mzima na mwenye buheri wa afya.

Lengo la kukutumia barua hii ni kukujulisha kuwa, wanafunzi wote wa darasa la sita watafanya ziara katika kiwanda cha kutengenezea maziwa. Kwa hivyo baba ninakuomba iwapo hali itakuruhusu, unitumie shilingi mia tano. Kiasi hicho kitanitosha kulipia nauli na hata kununulia pamba.

Mbali na hayo, mimi hapa ninazidi kujifunga nira curriculumni. Aidha ninazingatia nidhamu. Daima hujaribu juu chini kuzingatia mashauri yako kwani jungu kuu halikosi ukoko. Kamwe sitaki kusafiria mtumbwi wa mfinyanzi.

Tafadhali baba, wasalimie wote nyumbani. Waeleze sina neno na ninawapenda wote. Kwaheri baba mpendwa.

 

Mwana wako akupendaye,

 

(Sahihi)

Tumaini Njeri Kipande.

 

Zoezi:

  • Mwandikie rafiki yako barua umweleze jinsi ulivyoitumia likizo yako.
  • Mwandikie rafiki yako barua umwalike katika hafla nyumbani mwenu.
  • Andika barua kwa ndugu yako aliye katika shule ya bweni ukimjulisha hali ya mambo nyumbani Andkia barua kwa ndugu yako aliye katika darasa la nane. Mpe moyo na ushauri anapokaribia kuufanya mtihani wake.
  • Mwandikie mzazi wako barua ukimwelezea jinsi unavyoendelea na curriculum katika shule yako mpya.