Mwongozo wa kusahihisha

- Wakati wa kusahihisha insha za mtihani, alama hutuzwa kulingana na jinsi ambavyo mwandishi ameshughulikia kila kipengele miongoni mwa vipengele vitano vifuatavyo:

 • Maudhui
 • Msamiati na muundo
 • Mpango na mtindo
 • Mtiririko na mshikamano
 • Sarufi na maendelezo (tahajia)

- Kila kipengele huwa kimetengewa alama fulani. 

- Mtahini anastahili kutuza alama kwenye kila kipengele, kisha kuzijumlisha kwa usahihi ili kupata alama jumla.

- Basi ni vyema sana kila mwanafunzi aelewe vipengele hivyo ni vipi, na mahitaji ya kila kipengele. Hilo litamwezesha kujiandaa vilivyo.

 

Maudhui:

Ni hoja yaani mambo yanayozungumziwa, kuelezewa au kuhadithiwa kuhusiana na mada inayotakikana kuandikiwa insha. Katika kipengele hiki, mtahiniwa anatakikana kutunga mambo mengi kadri awezavyo na kuyafafanua vizuri. Ni muhimu sana mtahiniwa aonyeshe uwezo wake wa ubunifu. Katika kipengele hiki, mtahini ataweza kujua iwapo yalioandikwa ni ya akili ya kubuni. Ataweza kuamua iwapo uwezo wa ubunifu wa mtahiniwa ni wa juu ya wastani, wastani, chini ya wastani au amepotoka kabisa kwa kuandika jambo lolote kuhusiana na mada iliyokusudiwa.

Muhimu:
Mtahiniwa akinukuu au kunakili tu insha zilizotungwa na watu wengine na kudai ya kwamba ametunga insha, ni kujidanganya tu. Ieleweke waziwazi kuwa, katika uandishi wa insha, uwezo wa ubunifu wa mtahiniwa ndio hususan hutahiniwa. Mwanafunzi anashauriwa asiwe na mazoea ya kunukuu, kuadhukuru au kunakili ovyovyo tu insha zilizotungwa na watu wengine.

Katika kipengele hiki, mtahini hujiuliza maswali yafuatayo;-

 • Je, mtahiniwa ametoa maudhui yake kwa njia ya kuridhisha?
 • Je, ameyatoa maudhui ya kutosha, au ya wastani au machache sana?
 • Amepotoka kabisa? Alama zituzwazo katika kipengele hiki ni 14.

 

Msamiati na muundo:

Katika kipengele hiki, mtahiniwa huyaangalia yafuatayo kwenye insha:

 • Upo msamiati wa kuridhisha. Je mtahiniwa ameutumia msamiati wa hali ya juu au ulio sahihi?
 •  Je, msamiati huo unaambatana na yale anayozungumzia?
 •  Je, msamiati wake ni wastani au chini ya wastani?
 •  Je, amepamba lugha yake kwa methali, misemo, tashbihi, istiara na fani nyingine au amepachikapachika mambo hayo bila umakini?
 •  Je, miundo ya sentensi alizotumia ni ya kuridhisha? Sentensi zake zinaeleweka?

Muhimu:
Mtahiniwa anashauriwa atumie msamiati wa kiwango cha juu lakini anaouelewa barabara. Aidha, msamiati huo uambatane na yale yanayozungumziwa.Mtahiniwa anashauriwa kamwe asiyatumie maneno makubwa makubwa ilhali hayalingani na yale yanayoandikwa.

 

Mpango na mtindo:

Katika kipengele hiki, mtahini huangalia iwapo:

 •  Mtahiniwa ameyapanga mambo katika insha yake kwa njia inayoridhisha au ameyapanga ovyovyo tu.
 • Iwapo mtahini ametumia mtindo unaofaa kulingana na mada aliyopewa k.m. Je, iwapo ni insha ya barua, ameandika anwani, utangulizi, kiwiliwili n.k.? Alama zinazotolewa hapa ni 08.

 

Mtiririko na mshikamano:

Mtiririko ni mfuatano wa mawazo kutoka sentensi moja hadi sentensi nyingine, aya moja hadi ile nyingine na katika insha yote kwa jumla. Mshikamano ni ule mwambatano mzuri wa maelezo kutoka mwanzo wa insha hadi katika mwisho wake. Ili mtahini afikie uamuzi wa alama za kumtuza mtahiniwa katika kipengele hiki, atatakikana ajiulize:

Je, katika insha, upo mtiririko na mshikamano wa mawazo na maelezo kutoka sentensi moja hadi katika sentensi nyingine, aya moja hadi katika aya nyingine na katika insha yote kwa jumla.Alama zituzwazo hapa ni 03.

 

Sarufi na maendelezo (Tahajia):

Katika sehemu hii, mtahini huangalia iwapo mtahiniwa amezingatia sarufi ya lugha vilivyo au ameiharibu. Aidha huangalia iwapo ameyaendeleza kisawasawa maneno aliyoyatumia.Alama zinazotuzwa katika kipengele hiki ni 03.

Muhimu:
Mtahiniwa anashauriwa kuyaepuka matumizi ya maneno ambayo hana uhakika jinsi ya kuyaendeleza.

 

Mpangilio wa alama kulingana na vipengele

 • Maudhui 14
 •  Msamiati na muundo (ms/md)12
 •  Mpangilio/mtindo (mp/mt)08
 •  Mtiririko na mshikamano (mtr/msh)03
 •  Sarufi na tahajia 03
 • Jumla ya alama: 40

 

Mwongozo dira:

 • (01-04) Insha haieleweki kwani namna maneno yalivyopangika hayaundi sentensi zilizo na maana. Maneno ya Kiswahili yapo ila tu hayachangii maudhui kwa vyovyote. Mtiririko wa mawazo haupo. Kwa jumla insha imeandikwa vibaya.
 • (05-08) Insha imeandikwa vibaya. Mawazo hayajitokezi kwa urahisi. Yapo maneno ya Kiswahili lakini mengi yao yameendelezwa vibaya. Mawazo hayashikamani vizuri katika insha yote. Makosa ya sarufi pia ni mengi.
 • (09-12) Insha yaanza kueleweka. Mawazo ni mepesi sana. Msamiati ni wa chini ya wastani. Aya zipo ila udhaifu wa kupanga kazi kwa kiasi fulani unaonekana. Makosa ya sarufi na maenedelezo hasa ya kutenganisha na kuunganisha maneno yangali mengi.
 • (13-16) Insha yaeleweka. Maudhui yameshughulikiwa kwa wastani. Msamiati ni wa chini ya wastani. Kazi imepangwa kwa njia ambayo ni ya wastani. Makosa ya sarufi na maendelezo yangali mengi.

 

 • (17-20) Insha yaeleweka. Mawazo ni ya wastani na yanatiririka kuanzia mwanzo hadi mwisho. Msamiati ni wa wastani. Makosa ya sarufi na ya tahajia yameanza kupungua japo yangali mengi.
 • (21-24) Insha yaeleweka vizuri. Mawazo yanatiririka vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mawazo yanaanza kukomaa. Msamiati ni wa wastani. Tamathali za lugha kama vile methali, semi, tashbihi, tanakali za sauti n.k. zipo. Makosa ya sarufi na ya tahajia yapo.
 • (25-28) Insha yaeleweka vizuri. Mtiririko wa mawazo ni wa kuvutia. Ametumia mapambo ya lugha kama vile methali, tashbihi, nahau n.k. kwa wingi na kwa ufasaha. Insha yenyewe ina makosa machache ya kisarufi na tahajia.

 • (29-32) Insha yaeleweka vizuri. Ametumia lugha ya kiwango cha juu. Miundo ya sentensi inaridhisha. Mpangilio na mawazo unavutia. Msamiati alioutumia ni wa kiwango cha juu. Ametumia kwa ufasaha fani mbalimbali kama vile methali, istiara n.k. Urefu wa insha ni wa kuridhisha. Kwa jumla makosa ni machache mno.
 • (33-36) Insha yaeleweka vizuri. Anaimudu mada vilivyo. Anatumia lugha ya hali ya juu. Ubunifu ni wa kiwango cha juu. Amekomaa katika uandishi. Anatumia msamiati wa kiwango cha juu unaoonyesha kuwa anaitawala lugha. Urefu wa insha ni wa kuridhisha. Makosa ni machache sana.
 • (37-40) Insha yaeleweka vizuri. Anaimudu mada kabisa. Anatumia lugha ya kuvutia sana. Ana ubunifu wa hali ya juu. Anatumia msamiati wa kiwango cha juu sana. Anatawala lugha vilivyo. Anaipamba lugha kwa njia ya kuvutia sana. Urefu wa insha unaridhisha. Ni nadra kupata makosa katika insha yake.