KIFUNGU CHA 15

Kifungu cha kumi na tano Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.  

Uwanja ulikuwa umefurika pomoni alasiri hiyo. Timu ya Nguvu na ile ya Dhabiti zingepimana nguvu. Jogoo wa soka tarafani Kigumo angejulikana. Mashabiki wa miamba yote miwili walikuwa na furaha na buraha. Wachezaji nao waliteremka ugani kwa mikogo. “Leo ni leo, asemaye kesho ni mwongo. Asiye na mwana na aeleke jiwe.” Shabiki mmoja alisikika akisema. Mimi nilijinyamazia tu. Nilikuwa na uhakika kuwa timu yetu ingewafundisha Wananguvu jinsi ya kusakata soka. Hilo lilikuwa wazi kama mchana kwani uwanja ulikuwa wao na Wananguvu walionekana wanyonge. Hata sare zao hazikuwa za maana. Naam. Hayawi hayawi huwa. Kipenga kilipulizwa na mechi ikaanza. Pakawa na patashika pale uwanjani, kila timu ikijaribu kupata bao. Wachezaji wetu walionekana wakisakata ngozi kwa ufundi wa juu sana.

Walitoa pasi fupi fupi na za kasi ajabu. Ungesamehewa ungedhani walikuwa na spaki za kunasia mpira viatuni mwao. Wapinzani wao walionekana kubabaika. Mashabiki wao walinyamaza tu. Mnamo dakika ya saba, mchezaji wetu wa kiungo cha kati aliwapiga chenga walinda ngome ya Wananguvu na kupiga mkwaju kwa kasi. Maskini mlindalango alijipata akipiga mbizi upande wa kushoto huku mpira ukielekea kulia na kutulia wavuni. Shangwe na vigelegele vilihinikiza hewani. Tulizidi kuwahimiza wachezaji wetu wazidishe mashambulizi. Kocha wa Wananguvu alionekana na wasiwasi kama kuku mgeni. Alijaribu kuwashauri wachezaji wake akiwa kando ya uwanja. Hilo halikusaidia kwani dakika nne baadaye, mabao yalikuwa mawili kwa nunge. Wananguvu walijaribu kwa udi na uvumba kutafuta bao la angaa kuvutia machozi bila mafanikio. Ikawa ni sawa na kobe kukimbizana na duma.

Wachezaji wetu walianza kuongeza mikogo katika uchezaji wao. Muda wa mapumziko ulitimia na wachezaji wa pande zote mbili wakaondoka uwanjani. Baada ya kubwaga moyo na kupata ushauri, waliingia uwanjani. Dakika ya pili kipindi cha pili Wanadhabiti waliutingiza wavu tena. Licha ya mambo kuwa magumu, wapinzani wao walionekana kujitahidi vilivyo. Walijaribu kupenya ngome yetu bila ufanisi. Tulizidi kuwabeza kila mbinu zao zilipozimwa. Ghafla tu kama ajali, mshambulizi wa upande wa Nguvu alipata mwanya na kufunga bao kwa ustadi wa juu sana. Mlinda lango wetu alisimama tu huku mpira ukielekea wavuni. Mazingaombwe au nini? Wananguvu waliamshwa na bao lile. Walianza kuonyesha makali yao. Chenga zao zilituacha vinywa wazi. Kumbe reli na wembamba wake bado huweza kubeba gari moshi! Hakuna aliyeamini macho yake mchezaji yule yule alipotia kimiani bao la pili.

Kitambo tutulize mshtuko wetu, bao la tatu likatingwa. Mambo yakawa ni sare. Suluhu bin suluhu. Yote hayo tukayaona kama ndoto mbaya. Jinamizi. Waama, dunia ni rangi rangile. Wachezaji wetu walionekana kubabaika na kukasirika. Walisahau kuwa hasira ni hasara. Refa aliwaonyesha wawili wao kadi ya manjano kwa kuwatukana wapinzani wao. Mwengine alionyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya. Kumbe hasira za mkizi furaha ya mvuvi! Nahodha wa timu yetu alijiangusha karibu na lango la wapinzani akitarajia kufidiwa kwa penalti. Alipigwa na butaa alipoonyeshwa kadi ya manjano badala ya kuzawadiwa penalti. Kumbe ujanja wa nyani huishia jangwani! Aidha chiriku mzee hakamatwi kwa makapi. Refa alielewa mbinu zake. Kipenga cha mwisho kilipopulizwa mabao yalikuwa manne kwa matatu. Kweli kimya kingi kina mshindo mkuu baadaye.

Tulielewa kuwa kutangulia sio kufika na kamwe si vizurikukata kanzu kabla mwana hajazaliwa. Tuliwapongeza Wananguvu kwa ushindi wao kwani chanda chema huvishwa pete na asiyekubali kushindwa si mshindani.

 

Maelezo ya msamiati  

 • mikogo – maringo

 

1. Mwandishi alikuwa shabiki wa timu gani?        

 1. Nguvu.  
 2.  Dhabiti.      
 3.  Zote mbili.  
 4.   Hatujaelezwa.  

 

 

 2.wengi walionelea kuwa timu ya Nguvu ingeshindwa.

 

 1.  Wengi waaliamini kuwa timu ya Dhabithi ingeshindwa.  
 2.  Wachache waliamini kuwa Wananguvu wangeshindwa.  
 3. Wote waliamini kuwa timu ya Dhabiti ingeshinda.
 4. wa maoni ya wengi, hilo lilikuwa wazi kama mchana maana yake ni:        

3. Kwa nini wachezaji wa Nguvu walidharauliwa?    

 1. Hawakuwa na sare.
 2. Hawakuwa na siha.    
 3. Walikuwa wachache.  
 4. Walionekana kutokuwa na nguvu.

4. Kwa nini mlinda lango alipiga mbizi upande “ule mwingine?”

 1.  Aliuogopa na kuutoroka mpira.  
 2.  Alidanganywa na mfungaji bao.    
 3.  Hakuwa hodari katika mchezo.            
 4.  Alidhani mshambuliaji hangepiga mpira.

5. Ni wachezaji wangapi walioonyeshwa kadi ya manjano?  

 1. Wawili     
 2.  Watatu                
 3.  Wanne            
 4.  Hatujaelezwa

6. Kufikia wakati wa mapumziko, mabao yalikuwa mangapi kwa mangapi?            

 1.  Moja kwa bila.      
 2. Mawili kwa sufuri.  
 3. Matatu kwa mawili.    
 4. Manne kwa mawili.

7. Ni lipi hasa lililochangia kushindwa kwa timu shindwe?    

 1.  Hasira na maringo.  
 2.  Uzembe na kutojua kucheza.
 3.  Kutoshangiliwa na mashabiki. 
 4. Ukufunzi usiofaa.

8. Kwa nini mwandishi na wenzake waliachwa vinywa wazi?  

 1.  Mchezo ulikuwa wa hali ya juu na wa kuvutia.  
 2.  Mchezo ulishtusha sana.  
 3.  Walihofia kushindwa.       
 4. Walikasirika kwa kufungwa.

9. Bao la kusawazisha lilikuwa ni la ngapi?  

 1. La kwanza.      
 2. La tatu.    
 3. La nne.            
 4. La pili.

10. Nahodha wa Wanadhabiti alionyeshwa kadi kwa:  

 1.  kumwumiza mwenziwe.  
 2.   kutumia ujanja.
 3.   kuanguka katika eneo la hatari.    
 4.   kuunawa mpira.