Kifungu cha 20

Kifungu cha ishirini:  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Meja ni karani katika kampuni moja ya kibinafsi. Ni mwanamume wa umri wa makamu. Hata hivyo, yeye bado hupendelea mambo ya vijana. Si aghlabu umwone akiandamana au kutangamana na wanaume wa hirimu. Mtafute kuliko na vijana na bila shaka hutamkosa. Anachukia uzee. Anasikika mara nyingi akisema eti uzee ni haramu. Ni umri wa mateso. Meja hupendelea unadhifu wa nguo, mwili, chakula na makazi lakini si wa akili. Baadhi ya maneno na matendo yake hunuka hata kuliko mzoga uliooza. Maringo nayo yanamganda. Yeye na maringo ni sawa na fisi na tamaa. Maringo ni sehemu ya maisha yake. Meja amebarikiwa na mke na watoto wanne. Wao huishi mashambani. Huko analo shamba la urithi.

Licha ya kuwa na mshahara mnono, Meja haijali wala haibali familia yake. Ni mume na baba jina tu. Hajui watu wake wakalalaje wala wakaamkaje? Ametekwa bakunja na virukamito wa vijini. Anasa za mji zimemnasa. Amezama zii katika mto wa anasa. Mchana mmoja alitazama saa ukutani. Lo! Nusura achelewe kwenda kupata chamcha chake. Tayari akrabu ile fupi ilikaribia sana nambari moja nayo ile ndefu ikiwa juu ya nambari kumi. Alilikunja gazeti lake na kulitumbukiza mfukoni mwa koti lake. Siku hiyo alijihisi mchovu sana labda kutokana na maruweruwe baada ya mwisho wa juma wenye shughuli nyingi. Alijinyoosha na kuelekea nje ya ofisi yake. Pale pambajioni alimpata mhazili wake. Alimtupia tabasamu na kuelekea kwenye kambarau. Nje ya jumba lile watu walijaa kama kawaida.

Alipiga guu polepole kuelekea katika hoteli moja ya hadhi ya chini. Kwa kawaida alionekana katika hoteli ile wakati kama ule wa mwezi ambapo mfuko si mzito. Nyakati hizi nyingine alionekana katika hoteli za fahari. Ukweli ni kuwa, wahudumu wa hoteli ile walimchukia Meja. Ni vile tu hawangezikataa pesa zake. Aliwadharau, kuwatukana na kuwakemea kila alipoenda pale. Hasira zake za kutokuwa na pesa za kutosha alikuwa akizielekezea maskini wahudumu wake. Pale hotelini aliketi na kutazama ankara kwa muda kabla hajaagiza chakula chake. Pale bei ilikuwa rafi. Alikula chakula chake polepole. Alikimaliza na kutumbukiza mkono wake mfukoni. Lo! Mazingaombwe au jinamizi! Hakuwa na chochote mfukoni ila shajara yake. Kwa mara nyingine tena, masinzia walikuwa wamejinufaisha na jasho lake. “Mzee, tunakuelewa. Wacha mbinu zako eti umeibiwa.

Sisi ni chiriku wazee hatukamatwi kwa makapi. Leo, ujanja wako umeishia jangwani,” mhudumu mmoja tipwatipwa alimwelezea. Maskini Meja alijaribu kujitetea lakini yote yakawa ni bure bilashi. Alipewa masharti mawili. Avuliwe viatu na kurudi kazini au apewe kazi afanye huko jikoni kwa alasiri yote. Muungwana akivuliwa nguo huchutama. Meja, ukarani wake na maringo yake alielekezwa jikoni alipomenya viazi hadi machweo. Ungemwona ungedhani alikuwa akichimba kwa mikono yake. Maskini Meja alivuliwa nguo vilivyo. Alinyooshwa. Ukawa ndio mwisho wa kiburi chake. Akajua hakuna mume wa wote na kila mbwa ana siku yake. Maelezo ya msamiati maruweruwe – hali ya kujisikia dhaifu na hata kupata kisunzi pambajioni – mahali kama vile ofisini au hospitalini watu wanaposubiri kambarau – kreni, chombo cha kupandisha watu au vitu katika nyumba ya ghorofa nyingi mhazili

Maelezo ya msamiati

 • maruweruwe – hali ya kujisikia dhaifu na hata kupata kisunzi
 • pambajioni – mahali kama vile ofisini au hospitalini watu wanaposubiri
 • kambarau – kreni, chombo cha kupandisha watu au vitu katika nyumba ya ghorofa nyingi mhazili – sekretari
 • ankara – orodha ya vitu vilivyouzwa na bei zake;bili
 • bei rafi – bei ambayo haipunguzwi katu
 • shajara – kitabu kiandikwacho kumbukumbu za matukio ya mambo ya kila siku
 • makapi – maganda ya mbegu za mpunga
 • masinzia – wezi wa kuibia watu mifukoni bila ya wanaoibiwa kujua.

1. Ni maelezo yapi si sahihi kulingana na taarifa?  

 1.   Meja anayo familia.    
 2.   Meja si kijana.      
 3.   Meja na familia yake huishi mjini.   
 4.   Meja ana kiburi.

2. Ni sahihi kusema:      

 1.   Meja si mwadilifu.     
 2.   Meja ni maskini wa mali.      
 3.   Meja hana watoto.   
 4.   Meja huchukia anasa.

3. Kwa nini Meja haikimu familia yake?    

 1.   Hana uwezo huo.  
 2.   Hufuja pesa zake.      
 3.   Anaishi mbali sana na familia yake.   
 4.    Hana kazi wala bazi.

4. Kulingana na taarifa, Meja aliondoka ofisini saa ngapi?  

 1. Saa saba juu ya kitone.     
 2. Saa saba kasoro dakika kumi.     
 3. Saa moja na dakika kumi.  
 4.  Saa sita kasoro dakika kumi.

5. Kisawe cha pambajio ni:          

 1.   mapokeoni.        
 2.    sebuleni            
 3.    barazani        
 4.    hamamuni.

6. Ni kwa nini wahudumu wa hoteli ile hawakuvutiwa na meja?  

 1.   Hakulipa chakula chake.  
 2.   Aliwabeza.        
 3.   Alikula sana.    
 4.    Alikuwa mchafu.

7. Sentensi ipi sahihi?    

 1.    Meja aliikagua bili pale hotelini.  
 2.    Meja aliibiwa kila kitu alichokuwa nacho mfukoni.      
 3.    Pale hotelini, bei ya chakula ingepunguzwa.
 4.    Daima Meja alipata chakula chake pale.

8. masinzia walikuwa wamejinufaisha kwa jasho lake, maana yake ni:

 1. Meja alikuwa ameibiwa na majambazi.
 2. Meja alikuwa ametapeliwa na virukamito.  
 3. Meja alikuwa amefuja pesa zake.    
 4. Meja alikuwa ameathiriwa na wachopozi.

9. Kwa nini wahudumu walimwadhibu Meja?    

 1.   Kwa kukataa kulipia chakula alichotumia.
 2.   Kwa kuibiwa pesa zake.
 3.    Kwa kushindwa kulipia chakula alichotumiwa.    
 4.    Kwa kuwakosea heshima na kutolipia chakula alichotumia na.

10. Maskini Meja alivuliwa nguo vilivyo ina maana kuwa:

 1.  Meja alitolewa nguo na kubaki uchi.       
 2.  Meja alitishiwa kutolewa nguo abaki uchi.
 3.   Meja alifedheheshwa.            
 4.   Meja alitishiwa kuvuliwa viatu.