Kifungu cha 12

Kifungu cha kumi na mbili: Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yafuatayo.

Sikumbuki vizuri yapi yaliyokuwa yakiendelea akilini mwangu. Ukweli ni kuwa, mwili wangu ulikuwa umechoka. Akili zangu zilikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa nao moyo ulilegea. Haukuwa na nguvu za kukabiliana na mawimbi na misukosuko ya maisha. Nilikuwa nimeyatumbulia macho mlangoni. Pale nje palikuwa na vitoto vikicheza. Vilifanya niyatamani maisha yangu ya utotoni. Wakati huo sikuwa na majukumu mengi. Mawazo yangu yalikuwa mbali. Sikufuatilia yale yaliyokuwa yakiendelea kwenye kiredio pale kibagoni. Nami niliketi pale kitandani. Nilikuwa na njaa bali sikuwa na hamu wala nguvu za kukitayarisha kilalio. Hata kama ningekuwa na shauku ya kushtaki njaa, hapakuwa na chakula chochote pale. Nayo hiyo ingekuwa siku ya tatu mfululizo kulalia mate.

Si hayo tu, mwenye nyumba angefika wakati wowote kudai Kaisari apewe chake. Sikushughulika kujali iwapo angeniburuta nje au la. Nilidhamiria kumweleza avitwae vitu vilivyokuwa katika kijumba kile angalau afidie pango yake. Aidha, nilinuia kumwomba anipige jeki kwa kulipa nauli ya kusafiria hadi mashambani. Maisha ya mjini yalikuwa yamenichosha. Mkururo wangu wa mawazo na mikakati ulikatizwa ghafla na tangazo redioni. Yalitajwa majina ya wanaume watatu waliosemekana kuwa majambazi sugu. Walisemekana kuwa na silaha. Polisi walimwomba yeyote mwenye habari kuwahusu kuzitoa. Zawadi ingetolewa kwa kutoa habari ambazo zingewasaidia polisi kuwanasa nduli wale. Nilizinduka nikazivuta fikra zangu pamoja. Nikapata moyo wangu ukipapa, kijasho kikinitoka kwapani. “Macho …. Macho Mambo awe mwizi!” Nilijipata nikishangaa. Kweli yote yanga’aayo si dhahabu. Macho Mambo alikuwa ghulamu wa hirimu yangu.

Tulisoma naye katika shule ya msingi na kwa siku chache katika shule ya upili. Wavyele wake walikuwa na nafasi katika jamii. Aidha walikuwa waadilifu na wazingatifu wa nidhamu. Macho Mambo naye alikuwa na akili nyepesi, umbo zuri na mcheshi. Si siri kuwa nilikuwa nikiililia ngoa hali yake ya maisha. Nilipotamatisha curriculum yangu kutokana na uzito wa maisha, nilijipata nikibisha hodi kwao kupata vibarua angaa nizimbue riziki na nimchukue mamangu mkongwe. Nilifanya vibarua shambani mwa akina Macho Mambo kwa zaidi ya miaka minne. Macho alikamilisha curriculum yake na kujiunga na chuo kikuu. Wavyele wake walimwonea fahari si haba. Ujana nao ni umri wa kutisha. Una ndoto nyingi na nyingine za ajabu ajabu. Aghalabu nyingi za ndoto hizo huwa si chochote si lolote. Ni ulimbukeni tu.

Ndoto zangu ziliniongoza hadi mjini pindi tu nilipoacha vibarua kule kwa akina Macho Mambo. Nilinuia kwenda mjini na kuanzisha kiwanda changu binafsi. Niwe mkurugenzi. Ni ndoto ambayo hata leo husababisha niangue kicheko. Si kwa kuwa mtu kama mimi hawezi kuanzisha kiwanda chake. La hasha. Lisababishalo nicheke ni kasi ile niliyonuia kutekelezampango ule. Nilitarajia kutimiza ndoto ile kwa wiki mbili pekee. Aka! Huko mjini nilijipata nikiogelea katika mchanga moto. Nikawa ng’ombe aliyevunjika guu malishoni kiasi cha kutoweza kujikokota hadi zizini. Ni katika hali ile niliposhtushwa na habari zile za Macho Mambo. Mtoto aliyelelewa kwa hali na mali, tunu na tamasha, heshima na taadhima,. Lakini akakosa kuridhika. Waama, tamaa huua. Nikajituliza. Afadhali mimi. Licha ya njaa, nilikuwa na uhuru wangu.

Maelezo ya msamiati

 • tumbulia macho – angalia sana
 • hirimu – rika
 • kulalia mate – kulala njaa
 • lilia ngoa – tamani
 • pango – malipo ya nyumba ya kupangisha
 • tunu na tamasha – starehe tele
 • anipige jeki – anisaidie

1. Kwa nini mwandishi alikuwa amechoka mwili?

 1. Alitatizika maishani.        
 2. Alifanya kazi ngumu.                        
 3. Alikuwa mgonjwa.                      
 4. Alikuwa na njaa sana.

2. Ni sahihi kusema kuwa:    

 1. mwandishi alikuwa akisikiliza matangazo redioni.      
 2. mwandishi alikuwa akifurahia mchezo wa vitoto.  
 3. mwandishi alikuwa mgonjwa.      
 4. mwandishi alikuwa katika lindi la mawazo.

3. Je, mbona mwandishi hakuwa na hamu ya chakula?  

 1.  Hakuwa na chakula chochote.   
 2.  Hakuwa na njaa. 
 3. Alikuwa mgonjwa.  
 4. Alikuwa amechanganyikiwa kutokana na matatizo ya maishani.

4. Kwa nini mwandishi alipapwa na moyo na kutokwa na kijasho?    

 1. Alinuia kupata zawadi ya pesa.  
 2. Alihofia kushambuliwa na majambazi wale.    
 3. Alitambua jina la jambazi moja.              
 4.  Alishtuka kwa habari hizo zilizotangazwa.

5. Ni maelezo yapi sahihi?

 1.  Mwandishi aliyapata curriculum ya shule ya upili.  
 2.  Mwandishi alikuwa na tabia ya wizi.    
 3. Mwandishi alikuwa na tabia ya uzembe
 4. Mwandishi hakuwa na tabia ya mkono mrefu.

6. Mwandishi alikuwa na jukumu lipi bali na kujikimu?    

 1.   Kulipa kodi ya nyumba.              
 2.   Kumkimu mamaye.              
 3.   Kutoa zawadi ya pesa.      
 4.   Kununua chakula chake.

7. Macho Mambo aliingilia wizi kutokana na:      

 1. ugumu wa maisha nyumbani.        
 2.  tamaa za kujipatia makuu.                
 3. malezi yasiyofaa.                      
 4. ukosefu wa elimu shuleni.                     

8. Ni sentensi ipi sahihi?      

 1.   Macho Mambo aliingilia wizi pindi alipokamilisha curriculum yake ya shule ya upili.
 2.   Mwandishi aliingilia shughuli za vibarua baada ya kukosa karo ya shule ya upili.  
 3.    Macho Mambo alikuwa na ndoto ya kuanzisha kiwanda chake.          
 4.    Mwandishi alisoma hadi chuo kikuu.

9. Ni yapi yaliyosababisha mwandishi kuelekea mjini?  

 1.   Kutafuta vibarua.              
 2.   Kujiunga na chuo kikuu.            
 3.   Kuanzisha kampuni yake.        
 4.    Kutoroka wenzake.

10. Mbona mwandishi alikawia kurejea mashambani?      

 1.   Aliogopa kukamatwa.            
 2.   Alikuwa ameridhika na maisha huko mjini.        
 3.   Aliogopa kuchekwa na wenzake.          
 4.   Alikosa namna ya kusafiri hadi mashambani.