Kilimo

- Kilimo pia huitwa zaraa. Yafuatayo yanahusiana na kilimo.

1. Shamba/konde – sehemu itumiwayo kukuzia mimea.

2. Kichaka – sehemu iliyo na miti na nyasi. Sehemu isiyolimwa.

3. Weu/ucheu – sehemu ya ardhi iliyolimwa kwa kupanda.

4. Kwekwe/magugu – nyasi na mimea iliyoota pasi kupandwa na huathiri mimea mingine ambayo imepandwa.

5. Makoongo – mashimo au mitaro ya kupandia mbegu au miche.

6. Miche – mimea michanga.

7. Kituta/kitangu – sehemu ya kukuzia miche kabla haijapandwa.

8. Kuo – Mstari wa miche

9. Kitalu – sehemu ya kukaushia mbegu.

10. Ghala – sehemu ya kuhifadhia mavuno hususan nafaka kavu k.v. mahindi.

 

11. Kufyeka – kukata na kuondoa nyasi na miti.

12. Kung’oa visiki – visiki ni sehemu ya chini za miti; sehemu ya shina na mizizi. Kwa hivyo   kung’oa visiki ni kuziondoa ardhini sehemu hizo.

13. Kulima muauta – kulima huku ukiinua matuta ya udongo juu.

14. Kulima sesa – kulima huku ukilainisha udongo.

15. Kupalilia – kulima huku uking’oa kwekwe na magugu.

16. Kutayarisha makoongo – kutayarisha mashimo au mitaro ya kupandia mbegu au miche.

17. Kupanda sia – kupanda mbegu bila kutayarisha makoongo/mashimo.

18. Kupandikiza/atika – kuung’oa mche na kuupanda sehemu nyingine.

19. Kupogoa – kuyakata na kuyapunguza matawi ya miti.

20. Kunyunyizia – kumwagilia maji kwa utaratibu.

21. Kuvuna/kuchuma – kutoa mazao ya mimea shambani.

Aina za mbolea

 •  Mbolea ya mitambo
 •  Mboji/matanda
 •  Samadi Kilimo cha mifugo kinahusu ufugaji. Baadhi ya mifugo ni kuku, mbuzi, ngamia, punda,bata, kondoo ng’ombe n.k.

 

Msamiati kuhusu mifugo

1. Maksai - ng’ombe dume aliyehasiriwa na hutumiwa kuburutia plau.

2. Mbuguma - ng’ombe anayeendelea kuzaa.

3. Njeku - ng’ombe dume ambaye bado hajawa fahali.

4. Ndenge - mbuzi dume mchanga.

5. Beberu - mbuzi dume.

6. Mori - ng’ombe jike ambaye bado hajazaa.

7. Mtamba/mfarika/dacha - mnyama wa kike ambaye amekomaa lakini hajazaa.

8. Jogoo/jimbi - kuku wa kiume aliyekomaa.

9. Koo/mtetea - kuku wa kike ambaye amekomaa.

10. Tembe - kifaranga wa kike.

11. Pora - kifaranga wa kiume.

12. Kiweto - koo asiye na uwezo wa kutaga mayai.

13. Kutaga - kutoa yai kutoka kwenye kiloakia.

14. Kuatamia - kalia au lalia mayai kama afanyavyo kuku ili yaanguliwe.

15. Angua/totoa - toa vifaranga ndani ya mayai.

16. Kunyonyoa - kuondoa nyoya za kuku.

17. Pepea - weka matunda palipo na joto ili yaive.

18. Yai viza - yai bovu lisiloweza kuanguliwa.

19. Kiangulio/kitotoa - mtambo wa kuangulia mayai ya kuku.

 

Zoezi

Teua majibu sahihi ya maswali yafuatayo kitara, kisiki, kushika ardhi, hori, fuko, kucheua, samadi, ulingo, kuatamia, miche, kupogoa, kuvuna, winga, kupandikiza, kitalu makoongo, kunyauka, matanda, kunyonyoa pepea.

1. Sehemu kuku anapotagia mayai.

2. Chombo cha kulishia wanyama.

3. Mbolea itokanayo na kinyesi cha wanyama hususan wacheuao huitwa ________.

4. Ile hali ya kutafunatafuna chakula kitokacho tumboni kamavile wafanyavyo mbuzi huitwa ________.

5. Kitendo cha kuwafukuza ndege na wanyama wengine ili wasiharibu mazao shambani ni ________.

6. Jukwaa la kulindia shamba ili mazao yasiharibiwe na wanyama huitwa _____.

7. Mashimo ya kupanda mbegu.

8. Kile kitendo cha kuku “kuyalalia” mayai ili yaanguliwe huitwa _____.

9. Kupunguza matawi mtini ni _____.

10. Mimea michanga huitwa _____.

11. Kung’oa mimea michanga na kupanda sehemu nyingine ni _____.

12. Sehemu ya kukaushia mbegu.

13. Kishamba cha kukuzia miche kabla haijapandwa huitwa _____.

14. Hali ya mmea kufifia kutokana na joto au ukame ni ____.

15. Kipande cha mti kinachobaki chini ya ardhi baada ya mti kukatwa ni _____.

16. Hali ya mmea kuendelea kukua baada ya kupandwa ni _____.

17. Kitendo cha kutoa mazao/mavuno shambani ni _____.

18. Mbolea itokanayo na mlundikano wa majani makavu kwenye shina la mmea huitwaje?

19. Hali ya kuyaweka matunda palipo na joto ili yawe mabivu ni ____.

20. Kitendo cha kuondoa nyoya za kuku ni _____.

Vifaa vya kilimo

Kifaa 

Kazi

Fyekeo  Kufyekea nyasi
Jembe   Kuchimbia ardhi, kulimia.
Panga Kukatia miti, kuni.
Reki      Kuburura majani, kusawazisha udongo.
Haro    Kulimia.
Mundu    Kukatia miti.
Sepetu   Kuchotea mchanga.
Dodoki    Kusugulia mwili wakati wa kuoga.
Tingatinga  Kukokota vitu.
Glovu Kukingia mikono.
Shoka    Kupasulia kuni.
Plau    Kulimia.
Pigi    Kuangulia matunda.

 Panga

Fyekeo

Jembe

Sepetu

Plau

Reki

Shoka

             

Zoezi: Taja kazi ya vyombo vifuatavyo.  

1. Sepetu                   7. Reki

2. Jembe                    8. Panga

3. Muundu                 9. Tingatinga

4. Haro                      10. Fyekeo

5. Shoka                    11. Plau

6. Glovu                     12. Dodoki • Fyekeo by ebay used under CC_BY-SA
 • Jembe by Amazon used under CC_BY-SA
 • Panga by Knife Center.com used under CC_BY-SA
 • Plau by Jaipura agriculture used under CC_BY-SA
 • Reki by Chilling tools used under CC_BY-SA
 • Sepetu by Bulldog used under CC_BY-SA
 • Shoka by Ray Mears used under CC_BY-SA

 • Creative Commons License
  All work unless implicitly stated is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-NoDerivatives 4.0 International License.