Kifungu cha 19

Kifungu cha kumi na tisa Soma kifungu kifuatacho ujibu maswali.

Kila mwakani, simba wote walikuwa wakiangusha karamu. Hafla hiyo ilikuwa ikihudhuriwa na simba pekee. Hata hivyo, palikuwa na waalikwa spesheli ambao kazi yao ilikuwa ni kuandaa chakula na kutumbuiza. Mmoja wa waalikwa spesheli alikuwa sungura. Kazi yake ilikuwa ya kupiga gita. Kila mwaka, sungura alifurahia sana hafla ile. Kulikuwa na viburudisho vya kila aina. Nacho chakula kilikuwa tele na kitamu kama halua. Kila baada ya sherehe, sungura angepitia kwa msena wake fisi na kumhadithia yalojiri kwenye sherehe. Fisi angeyasikiliza yote hayo kwa masikitiko na majuto mengi. Kisa na maana, hakuwa na namna ya kufika shereheni mle. Naye sungura angempa pole. “Iwapo wewe ni rafiki yangu, mbona usinifanyie mpango niweze nami kufurahia uhondo ule hapo mwakani?”.

“Nitakusaidiaje na wewe mwenyewe ulijiharibia? Si kuna wakati ulipopata mwaliko na ukaenda? Mbona ukapigwa marufuku kurudi huko tena?” Sungura alilalamika. “Lakini kosa moja halimwachishi mke. Tafadhali nisaide tena,” fisi alizidi kulia. Baada ya majadiliano na ubadilishanaji wa mawazo, rafiki wale wawili walifikia uamuzi mmoja, sungura amfundishe mwenzake jinsi ya kupiga gita. Kwa miezi miwili mfululizo, sungura alijaribu juu chini kuhakikisha fisi ameuma uzi katika sanaa ya kupiga gita. Yote yakawa bure bilashi. Sungura akabwaga silaha. Ya gita yalipogonga mwamba, wakazua mbinu nyingine. Mnamo siku ile ya ndovu kumla mwanawe, fisi angevaa kama simba. Wangeitafuta ngozi ya simba, fisi aivae. Hivyo basi, sharti fisi angekuwa mwangalifu wakati wa kutembea huko shereheni. Vilevile, angepunguza uchu na ikiwezekana asiongee kamwe.

Yote yalienda sawa na hata siku ile ya sherehe, fisi akajumuika na wenzake. Pale shereheni, muziki uliponoga, fisi alishawishika kuanza kusakata rumba lakini akatolewa ishara ya tahadhari na sungura. Kamwe hakutaka kuvunjika guu. Alirejea kitini na kuketi. Wakati wa mlo ulipotimia, fisi alizisahau tahadhari zote na kukimbilia mlo. Mambo yalienda tege aliposahau yete ni simba na kuanza kukusanya mifupa yote iliyobakishwa na simba. Sungura alijaribu kumzindua rafiki yake lakini maji yalikuwa yamemwagika. Kitambo simba wazue mbinu ya kutegua kitendawili kilichokuwa mbele yao, fisi aliwategulia. Katika pilkapilka zile za kujikusanyia mifupa, ngozi ile aliyojitanda ilianguka. Alipoona hayo, alitimua mbio kuyanusuru maisha yake mfupa mmoja kinywani. Simba waliachwa wakivunjika mbavu.

Maelezo ya msamiati

 • uliponoga – ulipofikia kiwango cha juu
 • siku ya ndovu kumla mwanawe – siku ya umuhimu sana
 • ameuma uzi – anaelewa sana, ana ujuzi mkubwa

1. Ni kwa nini sungura alihudhuria hafla zile ilhali hakuwa simba?    

 1. Alikuwa na wajibu wa kupiga gita.    
 2. Alijifunika ngozi ya simba.              
 3. Alikuwa mpishi.                        
 4. Simba walipendezwa na wajihi wake.

2. Kila baada ya sherehe, sungura alikuwa akiyafanya yapi?  

 1.  Kula na kufurahia.    
 2.  Kumpitia rafiki yake fisi.   
 3.  Kumpelekea fisi makombo.
 4.  Kumshauri fisi.

3. Ni sahihi kusema:    

 1.   Fisi alikuwa ashahudhuriwa hafla kama hiyo awali.
 2.   Fisi hakuwahi kuhudhuria hafla kama ile hapo awali.
 3.   Fisi alijuana sana na simba.        
 4.   Maumbile ya fisi yanalandana na ya simba.

4. Ni nini maana ya ubadilishanaji wa mawazo?  

 1. Kutoania maoni ya kushauriana.       
 2. Kupiga soga.        
 3. Kulaumiana.            
 4. Kusikilizana.

5. Kwa nini fisi alikuwa amepigwa marufuku kutohudhuria sherehe?  

 1. Hatujaambiwa.  
 2. Kutokana na tabia zake mbaya. 
 3. Yeye hakuwa simba.         
 4. Hakuwa amejifunika ngozi ya simba.

6. Fisi akajumuika na wenzake ina maana:      

 1. Fisi akatangamana na fisi hao wengine walioalikwa.
 2. Fisi akatangamana na sungura kwenye sherehe.
 3. Fisi akabaki pweke.        
 4. Fisi akakaa pamoja na simba kwenye sherehe ile.            

7. Ni nini maana ya mambo yalienda tege kama ilivyotumika kwenye ufahamu?           

 1.    Mambo yalinoga.                    
 2.     Fisi alijisaliti.          
 3.     Fisi alionekana shereheni.  
 4.     Ngozi ilianguka.