Kifungu cha 14

Kifungu cha kumi na nne Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Kila mapambazuko, alionekana barabarani mbioni. Alikuwa akifanya mazoezi katika mbio za nyika. Jambo hilo alilifanya kwa ari na bidii zilizopita zile za mchwa. Alionyesha nia na azima ya kipekee. Kwa miaka mitano mtawalia, alichekwa na kubezwa na wengi pale kijijini Waliangua vicheko walipomwona akihema na kutweta huku jasho likimtiririka. Hayo yalimwumiza sana moyoni lakini akajinyamazia tu. Wengine walionekana kumhurumia kuwa huenda hakuwa na akili timamu. Wengine walisikika wakisema kuwa maskini Kaza alikuwa akiadhibiwa na Mungu. Ilisemekana kuwa akiwa mkembe wa umri wa karibu miaka kumi alitumwa akimbie dukani na mwendazake bibiye lakini akakataa. Eti akalaaniwa awe akikimbia kila asubuhi kama adhabu. Hakuna aliyekuwa na uhakika wa jambo lile.

Watu wengi hata walijiuliza mbona akaanza tabia hizo miaka mitano baada ya bibiye kwenda jongomeo? Baada ya mazoezi yake kabambe, Kaza alianza kushiriki katika mashindano mbalimbali. Aliposhiriki mara ya kwanza, hakufua dafu. Ajabu kubwa alishika mkia licha ya bidii zake zote. Kumbe bidii si pato! Alizidi kufanya mazoezi yake bila kufa moyo. Kadri alivyozidisha mazoezi yake ndivyo wengi walivyozidi kumcheka. Hakufa moyo. Alielewa kuwa penye nia ipo njia. Matendo yake yote haya waliyaona sawa na kuchota maji kwa pakacha. Mwaka uliofuata akiwa na umri wa miaka kumi na minane alishiriki tena katika mbio za nyika. Alipata nguvu mpya alipong’amua kuwa ingawa hakuibuka kuwa mshindi, hali yake ilizidi kuimarika. Alizidi kupata ujuzi. Hilo liliwasha moto wa ufanisi mtimani mwake. Aling’amua kuwa papo kwa papo kamba hukata jiwe.

Si ajabu basi, nusu ya mwaka baadaye, Kaza aliorodheshwa kwenye kikosi cha taifa cha kushiriki katika Michezo ya Olimpiki. Huo ukawa ndio mwanzo hasa wa kung’ara kwa nyota yake ya ufanisi. Nyota ambayo kwa miaka mingi ilikuwa haijang’ara kiasi cha kuonekana na wengi. Dunia nzima ilishuhudia Kaza akinyakua nishani ya dhahabu katika michezo hiyo ya Olimpiki. Kaza, kijana aliyelelewa katika kitovu cha ufukara, aliyebezwa na kutemewa mate, akajulikana kote duniani. Alivuliwa kofia hata na viongozi wa mataifa. Akawa mtu wa kutajwa. Mtu wa kula katika hoteli za fahari. Miaka wiwili baadaye Kaza akawa akinuka pesa. Maisha yake na ya aila yake yakabadilika. Akawasaidia wengi wa mbali na wa karibu. Waliomcheka awali wakakosa uso. Wakaelewa kuwa, dhamira ni dira na nia zikiwa pamoja, kilicho mbali huja karibu.

Maelezo ya msamiati

 • kutweta – kupumua kwa nguvu
 • mkembe – mtoto

1. Kwa nini wanakijiji wengine walikuwa wakimcheka Kaza?  

 1.   Hawakuelewa umuhimu wa mazoezi yake.  
 2.   Walimwonea huruma alipoyafanya mazoezi.
 3.   Walijua alikuwa akifanya jambo la ujinga.  
 4.   Walidhani alikuwa amelaaniwa.

2. Kulingana na baadhi ya wanakijiji, ni nani aliyekuwa akimwadhibu Kaza?

 1.  Mkewe Kaza.    
 2.  Nyanya yake Kaza.    
 3.  Mungu.      
 4.  Wazazi wake Kaza.

3. Kaza alianza kushiriki katika mashindano ya nyika akiwa na umri upi?  

 1. Miaka kumi.    
 2. Miaka kumi na mitatu.  
 3. Miaka ishirini.
 4. Miaka kumi na minane.

4. Ni methali ipi mwafaka kuelezea tabia ya Kaza baada ya kushindwa katika jaribio lake la kwanza?    

 1.  Kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa mapishi.  
 2.  Yakimwagika hayazoleki.                
 3.  Asiyekujua hakuthamini.            
 4.  Mbio za sakafuni huishia ukingoni..

5. Kwa nini Kaza alihisi uchungu moyoni?        

 1. Kwa kushindwa.     
 2. Kwa kubezwa na kuchekwa.  
 3. Kwa kuonewa.    
 4.  Kwa kulaaniwa.

6. Kushindwa kwa Kaza kulitokana na:  

 1.   Kutojiandaa vilivyo.     
 2.   Upinzani mkali.   
 3.   Umri mchanga.     
 4.   Ukosefu wa ujuzi.

7. Yote hayo waliyaona sawa na kuchota maji kwa pakacha, ina maana:  

 1. walimwona Kaza akilifanya jambo la ujinga.  
 2. walimwona Kaza kuwa mwendawazimu.  
 3. walimwona Kaza akijaribu kufanya jambo lisilowezekana.                              
 4.  walimwona Kaza kuwa mtu aliyepewa mambo makuu.

8. Mashindano ya Olimpiki huandaliwa baada ya kila miaka:  

 1. minne          
 2. mitano          
 3. miwili              
 4. kumi

9. Akawa mtu wa kula katika hoteli za fahari inamaanisha:

 1. Kaza akawa mpenda kula sana.    
 2. Kiwango chake cha maisha kikapanda ngazi nyingine.
 3. Kaza akawa mtu wa maringo.    
 4. Kaza akawa mtu wa kutalii hoteli kubwa kubwa.

10. Ni methali ipi isiyoweza kuelezea maendeleo ya Kaza?  

 1. Kuinamako ndiko kuinukako.    
 2. Msafiri ni aliye bandarini.                    
 3.  Mbio za sakafuni huishia ukingoni.
 4.  Penye nia ipo njia.