Kifungu cha 6

Kifungu cha sita Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuatia.

Katika aushi yangu shuleni, nilibahatika kufundishwa na walimu chungu nzima. Bila shaka wengi wao au niseme wote bado huwakumbuka. Mmoja wao aliyenifundisha ni mwalimu Rafaeli. Mwalimu Rafaeli alinifundisha katika shule ya msingi huko Wamahiga. Nilipojiunga na shule ya chekechea nilimpata huko na hata nilipohitimu curriculum ya msingi, nilimwacha huko. Ninaweza kusema kuwa nilianza kumfahamu zaidi mwalimu Rafaeli nilipokuwa katika darasa la nne. Alikuwa ni mwalimu wangu wa darasa. Fauka ya hayo, alinifundisha somo la Dini. Kwa wengine wetu, mwalimu Rafaeli alikuwa mwalimu wa kushangaza. Daima alikuwa mcheshi na mwenye bidii. Hata kutembea kwake kulionyesha ari yake. Nusu kutembea, nusu kukimbia. Lililotushangaza zaidi ni jinsi ambavyo alifanikiwa kufika shuleni mapema kuanzia Januari hadi Novemba.

Aliwatangulia walimu wote kufika shuleni. Hakujali iwapo alikuwa kwa zamu au la. Na kutofika shuleni je? Hilo lilikuwa jambo nadra na adimu ja barafu ya kukaanga iwapo si wali wa daku. Mara kwa mara tulishangaa, tulipigwa na butaa kwa kumwona akijikokota kufika shuleni licha ya kuugua. Mwalimu Rafaeli hakuchelea kutupatia wosia wa kila aina. Kila kukicha alituhimiza kujifunga nira, kuwa na nidhamu, heshima na kutumia raslimali kwa njia ya umakini. Alituhimiza kuutumia wakati wetu vizuri na kufanya mambo kwa kujitolea. “Hiari hushinda utumwa. Ifanye kazi kwa kuwa unamfanyia Mola wako.” Hayo yalikuwa maneno yake kila kukicha. Kuna jambo moja ambalo alinieleza na hata leo ninalikumbuka, “Hakuna awezaye kukulipa kwa huduma zako ila Muumba wako. Hata utakapoajiriwa, usifanye kazi kwa kuzingatia kiwango cha pesa utakazolipwa.

La hasha. Ifanye kwa bidii ili kumfurahisha Mungu aliyekupatia uwezo wa kuifanya amali hiyo.” Nako kuishi kwingi ni kuona mengi. Sasa hivi nimeyaamini maneno hayo. Ashakum si matusi, hakuna wakati wowote tulipomwona mwalimu Rafaeli na jozi mbili za viatu. Kila wakati alikuwa na jozi moja. Mashati yalikuwa mawili, suruali ndefu mbili na koti moja. Tai ilikuwa moja. Labda hayo yalikusudiwa kuwa funzo fulani. Daima, mavazi hayo yalikuwa safi na mwalimu wetu alionekana nadhifu. Huenda alitaka kutuonyesha kuwa hata bila kuwa na raslimali tele, bado mja anaweza kuishi maisha kamilifu. Chakula chake kilikuwa vivyo hivyo. Cha hadhi ya chini bali kilichotosheleza mahitaji yote ya kimwili. Si vitamini, si proteini, si wanga kilitosheleza yote. Mwalimu Rafaeli alijua kuongea. Maneno yake yalijaa busara na maono.

Si ajabu kuwa popote palipokuwa na sherehe au hata mazishi pale kayani, Rafaeli alialikwa kuongoza. Lililobaki kitendawili kwangu ni moja tu. Je, Ningemweka mwalimu Rafaeli wapi? Kati ya wakwasi au kati ya walalahoi pale kariani? Hata hivyo Rafaeli alitangamana na wote bila kizuizi chochote. Wakata kwa wakwasi, wasomi kwa wapuuzaji, mawalii kwa makafiri mabwana kwa watwana wote walisikizana na mwalimu Rafaeli.  

 

Maelezo ya msamiati

  • kujifunga nira – kujitahidi                                                                                                                           

1. Mwandishi anasema:            

  1.       Alifundishwa na walimu wengi bali humkumbuka mmoja tu.
  2.       Alifundishwa na walimu wengi na bado anawakumbuka.    
  3.       Alifundishwa na walimu wengi lakini Rafael alikuwa tajiri kupita wote.  
  4.       Alifundishwa na walimu wengi na wote walikuwa sawa.

2. Matembezi ya mwalimu Rafaeli yalionyesha:        

  1. Uzemb
  2. Bidii.
  3. Maringo.
  4. Kuchanganyikiwa.

3. Ni maelezo yapi sahihi kulingana na kifungu?  

  1.    Mwalimu Rafaeli alifika shuleni mapema wakati wa zamu yake.  
  2.    Mwalimu Rafaeli alikuwa mwalimu wa zamu kila wakati.  
  3.    Mwalimu Rafaeli hakuwahi kuwa mgonjwa.        
  4.    Mwalimu Rafaeli aliipenda na kuiheshimu kazi yake sana

4. Ni wakati upi mwandishi na wenziwe walikuwa wakipigwa na butwaa?          

  1.  Mwalimu Rafaeli alipofika shuleni.
  2. Mwalimu Rafaeli alipofika shuleni licha ya kuugua.
  3. walimu Rafaeli alipotembea haraka.  
  4. Mwalimu Rafaeli alipowachekesha.

5. Mwalimu Rafaeli alifurahishwa na wanafunzi wenye:  

  1. Bidii, nidhamu, heshima, uajibikaji na ridhaa.  
  2. Bidii, miigo, umakini, heshima na ridhaa.  
  3. Bidii, nidhamu, miigo na hiari.                      
  4. Bidii, uajibikaji, kiburi na heshima.

6. Ni sahihi kusema:  

  1. Mwalimu Rafaeli alikuwa mchafu.        
  2. Mwalimu Rafaeli alikuwa nadhifu.      
  3. Mwalimu Rafaeli alikuwa maskini.      
  4. Mwalimu Rafaeli alikuwa mvivu.

7. Mwandishi aliwasiwa yapi na mwalimu wake kuhusiana na kazi?  

  1. Kuhudumia dunia kwa kujitolea.            
  2. Kujibidiisha ili apate faida.                
  3. Kuyathamini malipo ya pesa kazini.    
  4. Kutotegemea malipo yoyote kazini.

8. Yaelekea mwalimu Rafaeli:      

  1.  Hakuthamini lishe bora.  
  2.  Hakuthamini unadhifu.                  
  3.  Hakuzingatia udaku wa watu.          
  4.  Hakuzingatia maadili.

9. Raslimali maana yake ni :      

  1. Utajiri wa mtu.      
  2. Mavazi ya mtu.  
  3. Uwezo wa mtu.  
  4. Matendo ya mtu.

10. Kichwa kinachofaa zaidi kwa taarifa hii ni?    

  1. Mwalimu Rafaeli.  
  2. Mwalimu wa ajabu.    
  3. Maisha mema.
  4. Umuhimu wa kuishi.