Kifungu cha 3

Kifungu cha tatu :Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yatakayofuatia.

Machwa hiyo niliwasili mastakimuni mwangu huku nimechoka tiki. Nilikuwa nimeshinda kazini kutwa nzima nikilibingirisha gurudumu la maisha. Amali yangu ilikuwa ya kuvunja mgongo. Hata hivyo, sikuwa na budi kuifanya kwani lisilo budi hubidi na mchagua jembe si mkulima. Kitambo kilalio kiwe tayari, nilijilaza pochini na kuanza kutazama runinga.

Msomaji wa taarifa ile alikuwa mwanamke aliyekuwa na sauti ya mwewe. Halikadhalika aliumbwa akaumbika. Hata hivyo, habari alizotupasha zilikuwa kinyume kabisa na maumbile ya mtangazaji yule. Habari zile zilikera, zikaatua moyo kisha zikahuzunisha. Nilipigwa na butwaa nilipokodolewa macho na picha za kitoto kilichokuwa na majeraha na makovu kote mwilini. Majirani walikizingira huku waandishi wa habari wakipiga picha majeraha yale.

Eti kilijeruhiwa na mzazi wacho! Kisa na maana kitoto kilipoteza shilingi kumi kilipotumwa cheteni! Wahenga walisema kuwa zunguo la mtukutu ni ufito. Aidha udongo uwahi ungali maji. Ni jambo la busara na hekima kumkanya mtoto na kumwelekeza. Ni sawa pia kumwadhibu mtoto iwapo mawaidha yanaonekana kugonga ukuta au kuambulia patupu. Lakini, ni unyama , ni uhayawani kumwumiza mtoto na kumtapikia cheche za matusi eti unamwadhibu! Adabu isiwe mateso.

Ni jambo la kuhuzunisha kuona kuwa, watoto wengi wanazidi kuumizwa na hata kuangamizwa na walezi wao. Ukiwauliza walezi hao, watakujibu eti wanawaelekeza watoto wao. Si ajabu kusikia wakisema eti wahenga walinena mcha mwana kulia hulia mwenyewe. Jambo moja ni bayana. Wengi wa watoto huwa hawana hatia wala taksiri. Lakini wanajipata wakielekezewa hasira na wazazi wao.

Hasira ambazo hawajui kiini wala chimbuko zake. Si ajabu kumwona mwanamume akilewa pombe na kuchokoza walevi wenzake. Anapopigwa, anaenda “kulipiza kisasi” kwa maskini mwanawe. Akiulizwa kwa nini akamchapa mwanawe atatoa visababu na visingizio chungu nzima. Kuanzia uzembe shuleni hadi kutotulia maabadini. Ah! Wito wangu ni mmoja tu. Watoto wapate haki zao. Kamwe watoto wasinyanyaswe, wasibezwe! Wasifanyizwe kazi za dhurubu na sulubu wala zile za shokoa. Kamwe wapewe mapenzi na haki za kujieleza.

Watoto wetu wanastahili nafasi na satua ya kutangamana na wenzao. Ninaomba watoto wetu wasigeuzwe kuwa vyombo vya kufanyia kazi. Wasiwe wanamgambo wa vita. Tafadhali wana wetu wasidhulumiwe kimapenzi wala wasitukanwe huku wakimithilishwa na kila aina ya vumbe. Ni vyema tukumbuke kuwa, jamii isiyo na kizazi cha usoni si jamii imara.

Ni jamii isiyo na mustakabali wowote. Iwapo basi tutakosa kuwa vielelezo kwao basi nao watageuka kuwa wanyama katika ngozi za binadamu. Waambao waliamba, mwana hutazama kisogo cha nina na mwana wa nyoka ni nyoka!

Maelezo ya msamiati:

  • mastakimuni – nyumbani, kiamboni, maskanini
  • amali – kazi
  • atua moyo – shtua
  • cheteni – sokoni
  • aksiri – dosari, ila
  • kazi za dhurubu/sulubu– kazi za kuchosha kazi za shokoa – kazi za kulazimisha 
  • satua – nafasi

1. Hoja kuu inayozungumziwa hapa ni ipi?

  1. Matangazo ya runinga.
  2.  Mtoto mwizi.
  3.  Adhabu kwa wahalifu.
  4.  Dhuluma dhidi ya watoto.

2. Nilipigwa na butaa nilipokodolewa macho na picha za kitoto kilichokuwa na majeraha na makovu mwilini, inamaanisha:

  1.  Kitoto kile kilinitazama.
  2.  Niliziona wazi picha za kitoto kilichodhulumiwa.
  3.  Nilizimia nilipoziona picha za kitoto kilichoteswa.
  4.  Nilikiona kitoto kilichojeruhiwa mbele yangu.

3. Mwandishi anaashiria kuwa:

  1.  Adhabu itolewe kwa uangalifu.
  2.  Adhabu kali kali zifuatwe na maonyo.
  3.  Kamwe adhabu zisitolewe.
  4.  Daima watoto washauriwe badala ya kuadhibiwa.

4. Mbali na kutopigwa, mtoto hastahili pia:  

  1.  Kutukanwa, kutapikiwa, kudharauliwa.  
  2.  Kutofanyizwa kazi ngumu, kulazimishwa kufanya kazi, kuchukiwa na kutukanwa.
  3.  Kupendwa, kufanyizwa kazi ngumu na za lazima, kutodharauliwa na kutoruhusiwa kutangaman na wenziwe.
  4.  Kutapikiwa cheche za matusi, kupigwa, kutopendwa na kufanyizwa kazi ngumu.

5. Watoto wasipolelewa vilivyo:

  1.  Watakuwa watu wa kutegemewa.
  2.  Huenda wasifikie malengo yao maishani.
  3.  Hawatajuta.
  4.  Watafua dafu maishani mwao.

 6. Ni maelezo yapi sahihi kulingana na kifungu?

  1. Kila wakati watoto huadhibiwa kutokana na utovu wa nidhamu.
  2.  Mara nyingine watoto huelekezwa hasira zisizowahusu ndewe wala sikio.
  3.  Si haki kumwadhibu mtoto.
  4.  Adhabu yoyote ile haimrekebishi mtoto kitabia.

7. Kwa kawaida wanaowaadhibu watoto visivyo:

  1.  Hujitetea
  2.  Hujuta
  3.  Hukamatwa
  4. Huwajibika

8. Mwana hutazama kisogo cha nina ni methali inayoeleza kuwa:

  1.  Kwa kawaida mtoto akiwa mgongoni huona kisogo cha mamaye.
  2.  Ni nadra mtoto kutofuata tabia za wazazi wake.
  3.  Si lazima mtoto afuate tabia za wavyele wake.
  4.  Kwa kawaida, mtoto hutofautiana na wazazi wake kitabia na kimaumbile.

9. ... watageuka kuwa wanyama katika ngozi za binadamu ina maana kuwa:

  1.  Watoto watakuwa wanyama.
  2.  Watoto watakuwa wakatili wasio na huruma.
  3.  Watoto watakuwa na maumbile ya wanyama.
  4.  Watoto watakuwa wakiishi katika mazingira sawa na wanyama.

10. Kulingana na mwandishi, ni wakati upi mtoto anapostahili kuadhibiwa?

  1.  Anapokosa. b. Anapofeli. c. Anapoiba. d. Anapopuuza nasaha.