Insha ya mazungumzo

- Insha ya mazungumzo huhusisha watu wawili au zaidi.

- Hali ya mazungumzo hutokea watu wawili au hata zaidi hujiingiza katika uzungumzaji.

- Mwanafunzi anapoandika insha ya mazungumzo sharti azingatie yafuatayo:

  • Insha yake sharti iwe na kichwa. Kichwa kitategemea wahusika wanaozungumza au mada wanayoizungumzia.
  • Majina au vyeo vya wanaozungumza. Kabla ya kila mzungumzaji au mhusika kuzungumza sharti jina au cheo chake kuandikwa. Kisha mazungumzo aliyoyatoa. k.m KARISA: Habari yako Kalume? KALUME: Nzuri ndugu Karisa. Umeshindaje? …
  • Uakifishaji. Alama za viulizi na za mshangao hutumika. Sharti mwandishi azitumie alama hizi ili kutoa picha halisi ya wale wazungumzaji. k.m. Ehe! Endelea. Ninakusikia. Mbona! Si yeye ni mwanawe?
  • Vitendo vinavyoandamana na mazungum•zo. Ni kawaida katika mazungumzo, wazungumzaji kujihusisha katika vitendo mbalimbali k.m kucheka, kulia, kutingiza kichwa, kunyoosha mkono n.k. Mambo haya huonyeshwa kwa maneno yanayofungiwa kwa mabano. Maneno haya yaliyo kwenye mabano hufuata pindi tu baada ya jina la mzungumzaji. k.m. JIRANI: (akitoa kalamu mfukoni) Tafadhali mtoto nieleze jina la mzazi wako.
  • Mabadiliko ya sauti. Iwapo mzungumza•ji atabadilisha sauti katika mazungumzo yake, sharti hayo yaonyeshwe kwa maneno katika mabano. MTOTO: (akinong’oneza) Mweleze ya kuwa nilizipoteza pesa huko uwanjani nikicheza.
  • Mazungumzo yanayokatizwa. Mara kwa mara mazungumzo huchacha kiasi cha wazungumzaji kukatizana maneno yao. Hali hiyo itokeapo, alama za dukuduku (…) hutumika kuonyesha kauli imekatizwa.k.m. MTOTO: Leo asubuhi ulipoondoka … MAMA: Asubuhi gani? Koma kudanganya!

 

Muhimu

Majina hayo huandikwa pambizoni mwa karatasi. Vilevile ni vizuri kuyaandika kwa herufi kubwa ili kuyatofautisha na mazungumzo yanayofuatia.

 

Muhimu

  •  Kwa vyovyote vile, unapoiandika insha yako, hakikisha mzungumzaji mmoja hayatawali mazungumzo kwa muda mrefu.
  • Ni jambo la muhimu sana mtahiniwa kuhakikisha kuwa mazungumzo yake yanafuata mada.
  • Mara kwa mara, ni vizuri mtahiniwa kutoa utangulizi mfupi ili kudokezea maudhui machache ya mazungumzo k.m. Mazungumzo yafuatayo ni kati ya Chifu na Mzee Hekima kuhusiana na mikakati ya kuimarisha usalama katika kitongoji cha Salama. CHIFU: …………………. MZEE HEKIMA: ………………
  • wapo mtahiniwa tayari amepewa majina ya wahusika katika mazungumzo yake, kamwe asiyabadilishe majina hayo. Vilevile, asiongeze majina ya wahusika wengine ambao hakupewa. Fauka ya hayo, mtahiniwa ahakikishe kuwa, kila mhusika aliyetajwa kwenye swali amehusishwa katika mazungumzo. Haijalishi hata kama atahusishwa mara moja tu.

Uangalie mfano ufuatao:

Uwahi udongo ungali maji.

Mwalimu: Habari yako Bwana Sema?

Sema: Njema sana mwalimu. Labda yako? Asante.

Mwalimu: Hata mimi sina neno. Ninashukuru. Ninachukua fursa hii kukushukuru kwa kuuitikia mwito wangu. Lengo hasa la kukuita hapa ni tuweze kuzungumza kuhusu tabia ya mtoto wako.

Sema: Asante sana mwalimu kwa kuchukua hatua hiyo. Kama wahenga walivyosema, kambare mkunje angali mbichi. Ni wajibu wetu sote kumwelekeza mtoto huyu. Tusisubiri hadi apotoke kabisa.

Mwalimu: Maneno yako ni ya ukweli mtupu. Jukumu la mwalimu na mzazi ni la umuhimu sana. Sharti sote tushirikiane ili tufaulu. Kama tujuavyo, umoja ni nguvu na mkono mmoja haulei mwana.

Sema: ……………………… Mwalimu: ……………………….

Zoezi

  • Andika mazungumzo yaliyotokea kati ya mama na shangazi walipokutana sokoni.
  • Andika mazungumzo yaliyotokea kati ya Daktari na mgonjwa katika wadi.