Kifungu cha 17

Kifungu cha kumi na saba Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Kila kukicha, katika kila pembe ya dunia, maneno ni yale yale vinywani mwa watawala na watawaliwa. Amani! Amani! Kila mmoja anasikika akihubiri ya amani duniani. Basi huenda ukapigwa na butaa mbona amani inazidi kuepuka dunia kama ukoma licha ya mahubiri hayo yote! Siku hizi mambo hata yamepita mipaka. Limezuka tatizo la ugaidi. Hali ya chuki imefikia kiwango cha juu hivi kwamba, wengine hata hujitolea mhanga kufa bora tu wamewaangamiza mahasimu wao. Ni kitendo cha kuatua moyo cha binadamu kufikia uamuzi wa kujiangamiza ili atimize ndoto yake ya kuwahiliki wenzake. Ni kitendo kinachodhihirisha chuki ya kina zaidi. Kitendo kinachoashiria kuvunjika moyo katika maisha.

Sidhani yeyote yule, mwenye ndoto na matarajio mema siku za usoni anaweza kufikia uamuzi wa aina ile. Aghlabu vitendo hivi hutokana na ile hali ya kutamaukiwa na tamaa ya kupata mema mbeleni. Dunia hii sasa si pahali salama tena pa kuishi. Kila tutembeapo, tunakumbwa na tisho la ugaidi. Hujui ni lini na ni wapi gaidi atatekeleza njama zake. Humjui adui yako. Huwezi ukajua nia za abiria mwenzako mliyeketi sako kwa bako katika matwana. Hujui lengo na dhamira ya mwenzako mnayenunua bidhaa pamoja pale sokoni au katika dukakuu. Wakati wowote anaweza “kulipuka” na mwangamie nyote. Swali ni hili: Ni nini kiini cha uhasama huu wote? Mbona insi wazidi kuangamizana na wote ni viumbe vya Mola? Kwani, maisha ya insi amekosa thamani na kuwa kama ya nzi?

Sababu chungu nzima zimetolewa kuhusiana na janga hili. Wengine husema eti ni tofauti za dini, wengine tofauti za rangi na hata zile za kiuchumi. Lakini ulipigapo darubini swala hili, utaona kuwa hayo yote ni visingizio visivyo na msingi wowote. Ukweli ni kuwa uovu huo wa ugaidi unatokana na kiburi, ubinafsi na mabezo ya binadamu. Iwapo waja wote wangenyenyekea, wawaheshimu wenzao, waongee kwa uwazi, wasiweke mahitaji yao mbele na kuyapuuza ya wengine, bila shaka suluhisho linaweza kupatikana. Hatuna haja ya kuwapigia wengine vifua. Hakuna faida yoyote kuwatolea wenzetu vitisho. Yafaa tuketi, tuzungumze tuelewane. Sisi sote ni binadamu wala sio hayawani. Sharti tukome katu kutafuta visingizio vya kuwanyanyasa wenzetu. Ni ujuha na ujununi kumdhulumu mwenzako eti kwa kuwa ngozi yake ni tofauti na yako.

Ni ubaradhuli kumhiliki mwenzako eti kwa kuwa imani zenu za dini hazifanani. Ni ubwege kumtesa mwenzio eti kwa kuwa si wa kabila lako. Ni upofu tu kumbeza mwenzako eti kuwa yeye ni hawinde wa mali au wa akili. Machoni mwa Muumba sote tu sawa. Maulana alituumba kwa mfano wake. Haya mengine yote ni mapambo tu.

 

Maelezo ya msamiati

  • mahasimu – maadui
  • kuwahiliki – kuwaangamiza
  • kutamaukiwa – kuishiwa na tamaa au matumaini
  • insi – binadamu
  • ujuha na ujununi  

1. Kulingana na taarifa, kwa nini amani haipatikani duniani?    

  1.   Watu hawajaelezwa mengi kuhusiana na amani.
  2.   Watu hawajajitolea vilivyo kudumisha amani.    
  3.    Watu hawazungumzi lugha sawa.
  4.    Watu hawana imani sawa za kidini.

2. Kitendo cha kujitoa mhanga kinaashiria:  

  1.  Chuki, hasira na ukosefu wa matumaini.  
  2.  Chuki, huzuni na majuto.              
  3.   Kero, ujinga na majuto.        
  4.   Ukosefu wa matumaini, kero na shufaka.

3. Kwa mujibu wa taarifa, ugaidi hutokana na:

  1. Tofauti za dini, kabila na uchumi. 
  2. Kiburi, ubinafsi na madharau.                    
  3. Ukabila na ujinga.                              
  4. Tofauti za rangi, uchumi na elimu.

4. Mwandishi anasema ni ujinga watu kuangamizana kwa kuwa:

  1. Sote ni viumbe vya Mungu na tu sawa mbele ya Muumba.    
  2. Sisi ni binadamu wala sio wanyama.  
  3. Sisi sote tuna mahitaji tofauti.  
  4. sisi sote ni waungwana.

5. Ni sawa kusema:

  1. Ni sawa kuwanyanyasa wenzetu bora tu tuna sababu
  2. Ni sawa kuwagandamiza wenzetu bora tu tutatoa visingizio.
  3. Ni sawa kuishi kama ndugu licha ya tofauti zetu. 
  4. Tofauti zetu zina umuhimu kuliko amani.

6. Mahasimu ni kisawe cha:  

  1. Rafiki    
  2.  Maadui    
  3.  Mtu            
  4.  Gaidi

7. Kwa nini mwandishi anafika uamuzi wa kuyalinganisha maisha ya binadamu na yale ya nzi?

  1.   Maisha ya binadamu hayana umuhimu mkubwa.
  2.    Binadamu wanazidi kuuana bila huruma.  
  3.    Binadamu na nzi huishi umri sawa.    
  4.     Binadamu anamchukia nzi.

8. Hatuna haja ya kuwapigia wengine vifua ina maana:  

  1.   Tusiwadharau, tusiwatishe wala tusiwapuuze wenzetu.    
  2.   Tuwatishe, tuwabeze na kuwagandamiza wenzetu.
  3.  Tuwapige wenzetu.        
  4.  Tusiwathamini wenzetu.

9. Mwandishi anasema kuwa si rahisi mtu wa aina gani kujitolea mhanga?

  1. Mtu mwenye hasira na chuki      
  2. Mtu mwenye matarajio mema ya baadaye
  3. Mtu mwenye imani yake                            
  4.  Mtu mchanga

10. Kinyume cha hawinde ni:

  1.  maskini            
  2.   kipofu          
  3.   tajiri              
  4.   mjinga