Kifungu cha 11

Kifungu cha kumi na moja Soma barua ifuatayo kisha ujibu maswali yafuatayo

Kijiji cha Imani, S.L.P. 49000, MARAGWA. 20.03.06. Kwa mwanangu mpendwa, Kwanza zipokee salamu tele. Ni matumaini yangu kuwa huko shuleni u salama salimini unapoendelea kulisukuma gurudumu la curriculum. Huna budi kufanya hayo auladi wangu kwani elimu ndiyo ngao maishani. Ni ngao ya kujikingia mawimbi ya uhawinde, ukupe na upuuzaji. Sisi hapa chengoni tu buheri wa afya. Nimekata shauri kukuandikia waraka huu baada ya kuipokea, kuisoma na kutathmini barua yako ya tarehe nane mwezi uliopita. Niliyasoma yote uliyonieleza. Mwanangu, wahenga walinena kuwa dalili ya mvua ni mawingu na penye moshi hapakosi moto. Maneno yako yanaashira mambo zaidi. Sina haja ya kukuficha mawazo yangu. Waambao waliamba, ukimstahi mke ndugu huzai naye. Nitakueleza kinagaubaga hisia zangu.

Maneno yote yako katika barua ile ni upuzi mtupu uliotokana na handaa za ujana. Kuniandikia barua eti hutaki kusoma kwa kuwa walimu wako wanakuchukia bure bilashi ni upuzi tu. Walimu wao hao wanaojitolea kukusomesha ili ufaulu aushini iweje tena wakuonee wivu? Wakuonee wivu kwa misingi ipi? Mwanangu hicho ni kiburi ulicho nacho. Sharti uelewe kuwa, wewe ni mtoto. Uwe tayari kukosolewa na kuelekezwa. Zikubali adhabu kwa roho safi. Kamwe usiwadharau walimu wako. Hao ndio wazazi wako huko shuleni. Uwakoseapo adabu, bila shaka hata sisi wazazi wako unatukosea. Walimu hao wana umuhimu mkubwa sana kwako. Mkubwa labda kuliko wetu sisi wavyele wako. Wana uwezo wa kukupatia elimu ya vitabu. Sisi hatuwezi. Elimu yetu ya vitabu bila shaka unaielewa.

Ninapozingatia hayo, hatimaye unanitumia barua iliyojaa upuzi na ulimbukeni wa ujana, bila shaka sharti nikasirike. Mwanangu, elewa mali niliyo nayo siyo yako. Usiitegemee kisha uyapuuze curriculum yako. Tafuta elimu kwani hiyo ndiyo mali isiyotekeka. Soma kwa bidii na uepuke handaa za ujana. Ujana ni fimbo ya mnazi, haudumu. Ujanani umri hatari uliofunikwa kwa ujinga na usipokuwa macho unaweza kukupotosha. Epuka kiburi kwa kila hali. Nyenyekea mbele za walimu wako. Elimu wanayokupatia itakuwezesha kujitegemea mnamo siku za usoni. Hakuna siku hata moja kiburi kitakulisha wala kikuvishe. Lakini elimu itakufanyia yote hayo iwapo tu utaipatia kipaumbele. Soma kwa bidii mwanangu. Ninajinyima mengi ili uelimike. Ninakata pua ili niunge wajihi. Isiwe basi badala ya kuunga wajihi unauguza kidonda. Mwanangu, yatilie maanani yote haya ili usijiume vidole siku za usoni.

Shirikiana na wenzako kwani upweke ni uvundo. Hata hivyo jiepushe na mikia ya mbuzi na masikio ya kufa kwani lila na fila havitangamani. Mama yako na ndugu zako wamekusalimia.

Babayo, Upuzi Kando.

 

Maelezo ya msamiati

  • auladi – mtoto mvulana
  • uhawinde – umaskini
  • ukimstahi – ukimheshimu
  • handaa – danganya
  • ulimbukeni – hali ya kupata au kutumia kitu kwa mara ya kwanza

1. Mwandikiwa alikuwa:     

  1.  mtoto wa kike.   
  2.  mtoto wa kiume.   
  3.  mtoto wa kipekee katika familia.        
  4.   mtoto yatima.

2. Lipi lililomsababisha mzazi kumwandikia mwanawe barua?

  1. Hamu ya kumjulia hali mwanawe.      
  2. Nia ya kumshauri mwanawe.  
  3. Maendeleo ya mwanawe shuleni.    
  4. Maudhui ya barua ya mwanawe ya hapo awali.

3. Ni sahihi kusema, mwanafunzi mhusika ni:

  1. mtiifu bali ni mwongo.                  
  2.  ana kiburi ila ana bidii.                    
  3.  mnyenyekevu na mpole.      
  4. mwenye kiburi na mjanja.

4. Ukimstahi mke ndugu huzai naye ina maana:

  1.   baba alinuia kumweleza mwanawe ukweli wote.  
  2.   baba hakunuia kumweleza mwanawe ukweli wote.        
  3.   baba hakumwogopa mwanawe.      
  4.   baba alimwonea mwanawe aibu.

5. Kwa mujibu wa baba mtu, mwanawe:  

  1. alikuwa akipotoshwa na wenziwe.        
  2. alikuwa akipotoshwa na ujana.                  
  3. alikuwa akipotoshwa na walimu.    
  4. alikuwa akipotoshw na anasa.

6. Ni elimu ipi baba anampatia mwanawe?      

  1. elimu ya vitabuni.  
  2. elimu ya upuzi      
  3. elimu ya dunia    
  4. elimu ya bure

7. Ni sahihi kusema:  

  1.  baba anamwelimisha mwanawe bila ugumu wowote.        
  2.  baba anajinyima mengi ili amwelimishe mwanawe.        
  3.  baba hathamini elimu                                                    
  4.  baba anawalaumu walimu wa mwanake.

8. Katika kifungu hiki, walimu wanamithilishwa na:

  1.   baba             
  2.   wajuzi            
  3.   vijana            
  4.    wazazi

 

9. Hakuna siku hata moja kiburi kitakulisha au kikuvishe inamaanisha:    

  1.   kiburi huangamiza maisha ya mhusika.    
  2.   kiburi hakimnufaishi yeyote kwa lolote lile.  
  3.   kiburi hudanganya.                      
  4.    kiburi huleta majuto.

10. Baba mtu anamtahadharisha mwanawe kutoandamana na:

  1. walimu wake.  
  2. wanafunzi wenzake.   
  3. vijana wote.  
  4. vijana wazembe na watukutu.