Ngeli ya A - WA

Viambishi rifa/ngeli vya vikundi hivi ni kama vifuatavyo

A - WA

Mwanafunzi anasoma kwa bidii. Wanafunzi wanasoma kwa bidii. Nyoka ameingia shimoni. Nyoka wameingia shimoni. Kiroboto ameruka. Viroboto wameruka.

 

KI - VI

Kitabu kinapendeza. Vitabu vinapendeza. Chombo kimetia nanga. Vyombo vimetia nanga.

 

LI - YA

Jiwe limerushwa. Mawe yamerushwa. Jitu limefika. Majitu yamefika.

 

I - ZI

Nguo imeshonwa. Nguo zimeshonwa. Sahani imepanguzwa. Sahani zimepanguzwa.

Ngeli ya A - WA

Ngeli hii hujumuisha nomino zote ambazo zikitumika katika sentensi na sentensi hizo ziwe na kiarifa, kiambishi cha kiarifa hicho kitakuwa a (umoja) na wa (wingi).

Baadhi ya hizi nomino ni zile za viumbe vyote ambavyo vina uhai katika hali ya kawaida (wastani (isipokuwa mimea) kama vile watu, wanyama, wadudu, samaki, vimelea vya wadudu na ndege.

Vivumishi

Kila ngeli inazo sheria zake. Sheria hizi tunaweza kuziita vivumishi. Vivumishi hivi hubadilika kutoka ngeli moja hadi nyingine.

Kiwakilishi amba-

Hutumika kusimamia nomino au kitenzi katika sentensi. Kiwakilishi hiki hubadilika kutoka ngeli moja hadi nyingine. Kwa kawaida, kiwakilishi amba hufuata nomino au kitendo kinachojulishwa au kinachohusika.

  • Umoja: Mbuzi ambaye anacheua ni wangu.
  • Wingi: Mbuzi ambao wanacheua ni wetu.

“O” rejeshi

Kivumishi hiki hutumika kurejelea nomino na pia kitenzi. Kinatumika badala ya kiwakilishi amba-.

  • Umoja: Mbuzi anayecheua ni wangu
  • Wingi: Mbuzi wanaocheua ni wetu.

Kwa kawaida “o” rejeshi hutumika mwishoni mwa kitenzi katika wakati wa mazoea.

k.m. Msomi ambaye hujitahidi hufanikiwa – Msomi ajitahidiye hufanikiwa.

“O” rejeshi inaweza pia kutumika katikati ya kitenzi. Katika wakati ujao, “o” rejeshi inapotumika katika kitenzi, silabi ka huongezewa kabla ya “o” rejeshi.

k.m. Mgeni ambaye atafika ni wa mbali – Mgeni atakayefika ni wa mbali.

Muhimu Ni makosa kutumia kiwakilishi amba pamoja na kirejelei ‘o’ kurejelea au kuwakilisha nomino moja.

 

Ndi- ya kusisitiza

Hutumiwa kutilia mkazo kuhusu lile linalozungumziwa.

  • Umoja: Mbu huyu ndiye aliyenyunyiziwa dawa.
  • Wingi: Mbu hawa ndio walionyunyiziwa dawa.

 

Si- ya kukataa

Hutumiwa kukanusha ndi- ya kusisitiza.

  • Umoja: Mbu huyu siyealiyenyunyizi-wa dawa.
  • Wingi : Mbu hawa sio walionyunyizi- wa dawa.

 

Na- ya kirejelei

Hutumiwa pamoja na silabi kurejelea nomino au kitenzi kinachozungumziwa.

  • Umoja: Chiriku huyu naye ananisumbua.
  • Wingi: Chiriku hawa nao wanatusumbua.

 

Vivumishi vya viashiria/vionyeshi

Viashiria hutumika kuonyeshea mahali nomino au kitenzi kipo kama vile karibu, mbali kidogo na mbali sana Vipo viashiria vitatu katika kila ngeli:

i) kiashiria cha kwanza (karibu)

ii) kiashiria cha pili (mbali kidogo)

iii) kiashiria cha tatu (mbali sana)

Katika ngeli ya A-WA viashiria hivyo ni: karibu mbali kidogo mbali sana

Umoja: huyu huyo yule

Wingi: hawa hao wale

 

Muhimu Kiashiria cha kwanza kwa kawaida hakitumiki katika wakati uliopita au wakati ujao. Uandikapo wingi, sharti kiashiria kidumishe nafasi yake (k.m wingi wa huyo ni hao wala hauwezi kuwa hawa au wale).

Hutumika kutilia mkazo zaidi.

Umoja: yuyu huyu yuyo huyo yule yule

Wingi: wawa hawa wao hao wale wale

 

Viashiria radidi

Hutumika kutilia mkazo kwa kurudia kiashiria kile kile bila mabadiliko yoyote. Badala ya kusema mtoto huyu unasema mtoto huyu huyu.

Umoja: huyu huyu huyo huyo yule yule.

Wingi: hawa hawa hao hao wale wale.

 

Vivumishi vya pekee

Vipo vivumishi vya pekee sita: -enye, -enyewe, -ote, -o-ote, -ingi, -ngine.

Kivumishi - enye

Kivumishi - e n y e hutumika kuonyesha kumiliki (kuwa na) nomino. Kwa kawaida, kivumishi - enye hufuatwa na nomino iliyomilikiwa.

  • Umoja: Mja mwenye bidii hufua dafu aushini.
  • Wingi: Waja wenye bidii hufua dafu aushini.

Muhimu.

Ni makosa kivumishi -enye kufuatwa na kitenzi au kiarifu k.m. Mwalimu mwenye anafundisha ni makosa. Inastahili kuwa: Mwalimu ambaye anafundisha au mwalimu anayefundisha.

 

Kivumishi -enyewe.

Hutumika kuonyeshea:

a) nomino au hali ile ile iliyotarajiwa. k.m. Mgeni mwenyewe ndiye huyu. (Yaani si mgeni mwengine bali ni yule yule aliyetarajiwa).

b) hali ya kutoingiliwa kwa jambo. Yaani jambo limetendeka bila kuingiliwa. k.m. Mtoto ameanguka mwenyewe.

c) Humaanisha anayemiliki kitu k.m. Wino huu una wenyewe. K.m. Zi wapi nguo? Zimechukuliwa na wenyewe.

  • Umoja: Mwanafunzi mwenyewe ana bidii.
  • Wingi: Wanafunzi wenyewe wana bidii. au
  • Umoja: Amekipika chakula mwenyewe.
  • Wingi: Wamevipika vyakula wenyewe.

Hutumika kuonyeshea kila kitu (bila kubakia au kubagua)

Wingi: Mijusi wote wameangamizwa.

Muhimu

Katika ngeli ya A - WA, kivumishi -ote hakitumiki katika umoja.

 

Kivumishi -o-ote

Hutumiwa kuonyeshea mojawapo ya nomino.

  • Umoja: Nitamnunua kuku yeyote.
  • Wingi: Tutawanunua kuku wowote.

 

Kivumishi -ngi

Hutumika kuonyeshea hali ya utele.

Wingi: Mvuvi aliwavua nswi wengi.

Muhimu

Katika ngeli ya A - WA, kivumishi -ngi hutumika pamoja na kielekezi cha nomino Mfano: Mwingi wa akili.

 

Kivumishi -ngine

Hutumika kuonyeshea zaidi ya au tofauti.

  • Umoja: Shangazi amejifungua malaika mwengine.
  • Wingi : Kina shangazi wamejifungia malaika wengine.

Vivumishi vya visifa vya idadi

  • Visifa hivi huonyeshea idadi ya nomino husika. Visifa huchukua viambishi tofauti tofauti kulingana na nomino zinazohusika.
  • Hata hivyo, kunavyo visifa vya idadi visivyobadilika kama vile sita, saba, tisa, kumi, mia, elfu, milioni.
  • Katika ngeli ya A-WA, visifa vya idadi huchukua viambishi kama ifuatavyo. mmoja sita kumi na mmoja wawili saba kumi na wawili watatu wanane kumi na watatu wanne tisa kumi na wanne watano kumi ishirini n.k.

 

Kiulizi -ipi?

Hutumika kujua ni nomino gani?

  • Umoja: Ni mjumbe yupi aliyekupasha habari hiyo?
  • Wingi: Ni wajumbe wepi / wapi waliowapasha habari hizo?

 

Kiulizi -ngapi?

Hutumika kuulizia idadi.

Wingi : Darasani muna wanafunzi wangapi?

Muhimu

Kiulizi ngapi hutumika tu katika hali ya wingi.

 

Muhtasari

• Kiwakilishi a m b a– na ‘ o ’ rejeshi vina jukumu moja. Kwa hivyo havitumiki vyote viwili kwa pamoja.

• Vivumishi vya kwanza vitano, yaani amba-, ‘o’ rejeshi, ndi- ya kusisitiza, si- ya kukataa, na na- ya kirejelei vina mizizi kutoka kiwakilishi amba-(ambaye, -ye-, ndiye, siye, naye)