Uhusiano wa watu na nchi

- Nchi au taifa lolote lile sharti liwe na watu.

- Wengine wamezaliwa pale, wengine wakahamia pale na wengine wamefika kwa shughuli za kazi. Hivyo ni kusema, katika nchi yoyote, kila raia ana uhusiano fulani wa kitaifa.Yatazame yafuatayo:

1. Mtu aipendaye nchi yake na yu tayari kuipigania ni mzalendo.

2. Mtu ambaye anaichukia nchi yake na hata anatoa siri kwa adui ni msaliti.

3. Mtu aliyekimbia nchi yake kutokana na matatizo kama vile njaa na vita ni mkimbizi.

4. Mtu ambaye ameitoroka nchi yake labda kutokana na sababu za kisiasa ni mtoro.

5. Mtu ambaye ametembelea nchi yake kwa madhumuni ya kujionea na kustarehe ni mtalii.

6. Mtu ambaye anapeleleza mambo ya nchi nyingine kisirisiri ni jasusi.

7. Mtu ambaye anaiwakilisha nchi yake katika taifa jingine ni balozi.

8. Mtu ambaye ameihamia nchi nyingine na kuyafanya makao yake huko ni mlowezi/setla.

9. Mtu ambaye anaitawala nchi nyingine isiyo yake ni mkoloni au mbeberu.

10. Mtu ambaye ameanzisha jambo kwa mfano mapinduzi ni mwanzilishi.

 

11. Mtu ambaye amezaliwa katika nchi fulani ni mzaliwa.

12. Mtu ambaye amezaliwa mahali fulani na akaendelea kukaa hapo ni mwenyeji.

13. Mtu ambaye maskani yake ni kijijini ni mwanakijiji.

14. Mtu ambaye maskani yake ni mjini ni mwanamji.

15. Raia aliyejitolea kufanya kazi ya ulinzi ni mwanamgambo.

16. Mwenyeji wa nchi fulani ni mwananchi.

17. Mtu ambaye anatumiwa na kiongozi mwengine kwa manufaa ya kiongozi ni kibaraka au karagosi.

18. Mtu anayeamini na kuendeleza vitendo vya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ili watu wengi wanufaike ni mwanamapinduzi.

19. Mtu anayefuata mfano wa kisiasa wa utawala wa mabavu ni fashisti.

20. Mtu asiyependelea mabadiliko ni mhafidhina.

21. Mtu anayetangulia kuanzisha jambo ni mtakadamu.

 

Zoezi

Toa majibu sahihi. mtetezi, mhajiri, mhaini, mgombezi, mgunduzi, wakimbizi, mhafidhina, jasusi, mwanamgambo, karagosi.

1. Mtu ambaye amehamia mahali kutoka sehemu nyingine ni ________.

2. Mtu ambaye amedhihirisha jambo ambalo halikuwa likijulikana ni ________.

3. Mtu anayefanya njama za kupindua serikali yake ni ________.

4. Mtu anayemtetea mwengine ili apate haki yake na asionewe ni ________.

5. Mtu anayewania nafasi ya uongozi kwa kushindana na wengine ________.

6. Mtu ayapingaye mabadiliko huitwa ________.

7. Watu waliotumiwa na wakoloni kuwagandamiza Waafrika wenzao enzi za ukoloni wanaweza kuitwa ________.

8. Kutokana na kudidimia kwa usalama, Juma na wenzake wamejitolea kulinda kijiji chao. Tunaweza kuwaita ________.

9. Mzee huyo alitiwa mbaroni akipeleleza kambi za wanajeshi wetu. Yeye ni ________.

10. Kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, nchi yetu ilipokea ________ wengi kutoka nchi jirani.  • ambassodor by Unknown used under Creative Commons Attribution-NonCommercial-NoDerivatives 4.0 International License
  • wakimbizi by Unknown used under Creative Commons Attribution-NonCommercial-NoDerivatives 4.0 International License
  • watalii by Unknown used under Creative Commons Attribution-NonCommercial-NoDerivatives 4.0 International License

  • Creative Commons License
    All work unless implicitly stated is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-NoDerivatives 4.0 International License.