Biashara

Biashara inahusu ununuzi na uuzaji wa bidhaa na/au huduma.

Mifano ya bidhaa ni kama vile nguo, magari, chakula n.k.

Mifanol ya huduma ni kama vile bima, simu n.k.

Kwa kawaida lengo la msingi la kufanya/kupiga biashara ni kupata faida ingawa mara kwa mara, hasara hupatikana.

Biashara inaweza kuwa ya kitaifa (hufanywa katika taifa moja) na pia ya kimataifa (hufanywa baina ya mataifa zaidi ya moja).

Msamiati wa biashara

1. Faida/tijara/kivuno/chumo/ziada - Pato libakialo baada ya kuondoa gharama za kufanya biashara k.v. ununuzi na usafirishaji.

2. Hasara -Ukosefu wa faida; Hali ya kupoteza pato au mali katika biashara.

3. Bei -Kiwango cha pesa kununulia au kuuzia bidhaa au huduma fulani.

4. Uuzaji wa rejareja -Uuzaji wa kiasi kidogo kidogo.

5. Uuzaji wa jumla - Uuzaji wa kwa pamoja.

6. a) Bei rafi - Bei ambayo haipunguzwi.

b) Kipimo rafi - Kipimo ambacho hakipunguzwi.

c) Bei ya kuruka - Bei isiyokubalika kisheria/haramu.

7. Raslimali - Ujumla wa mali yaanyomilikiwa na mtu au nchi.

8. Malighafi -Mali yanayotumika kutengeneza vitu vingine k.m. pamba ni malighafi ya kutengenezea nguo.

9. Maliasili -Utajiri kama vile madini, misitu, maziwa, mito, anga vinavyopatikana katika mazingira.

10. Uwekezaji - Kutumia pesa/mali ili kuzalisha fedha/mali zaidi.(ilikupata faida).

 

11. Kitegauchumi - Rasilmali k.v. kiwanda inayotumika kuzalisha mali.

12. Ujasiriamali -Uwekezaji mtaji katika biashara.

13. Mtaji -Mali ya kuanzisha biashara au kuipanulia.

14. Ulanguzi -Ufichaji wa bidhaa ili bei yazo iruke.

15. Magendo -Upigaji biashara kwa njia haramu/isiyo halali.

16. Chenji -Pesa zinazobaki baada ya kununua kitu.

17. Maduhuli - Bidhaa ambazo hununuliwa kutoka nchi za nje.

18. Mahuruji - Bidhaa zinazouzwa nchi za nje.

19. Ushuru - Kodi ya kuingiza bidhaa nchini au kuziuza/Ada ya forodha.

20. Ruzuku - Pesa zinazotolewa na serikali kwa idara mbalimbali ili kujiendeleza.

 

21. Mshtiri - Mnunuzi.

22. Mteja - Aendaye kununua bidhaa au huduma.

23. Wakala - Ajenti.

24. Utandawazi -Utaratibu wa mataifa kushirikiana katika nyanja mbalimbali k.v. biashara.

25. Ubinafsishaji -Hali ya kusababisha mali ya umma imilikiwe na watu binafsi.

26. Ubia -Ushirikiano wa watu wawili au zaidi katika shughuli k.v. ya biashara.

27. Hawala - Hundi/cheki.

28. Amana - Kitu unachomwekea mwenzako hadi atakapokihitaji.

29. Turuhani/kipunguzo – Kiwango kinachotolewa kutoka katika bei iliyotangazwa.

30. Ikfisadi -Uangalifu katika kutumia fedha/mali.

31. Ubepari -Mfumo wa uchumi ambao unawawezesha watu wachache kumiliki raslimali na vitegauchumi.

32. Ukiritimba -Hali ya kuzuia wengine kufanya biashara au kushindana katika biashara.

33. Dukakuu - Duka kubwa ambapo wateja hujichukulia bidhaa watakazo kutoka rafuni.

34. Hisa - Sehemu ya mtaji katika biashara.

 

Zoezi: Eleza maana ya maneno yafuatayo.

1. Chenji

2. Piga bei

3. Tia bei

4. Patana bei

5. Mrabaha

6. Mgavi

7. Keshia

8. Mkopo

9. Keshi

10. Uzalishaji