Nyakati

Wakati ni kipindi fulani cha muda. 

Kwa kawaida kuna wakati wa mchana na wakati wa usiku. Mchana huanzia jua linapochomoza hadi linapozama. Mchana huupisha usiku.

Kipindi cha usiku huendelea hadi jua linapochomoza. 

Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, kipindi cha mchana huchukua saa kumi na mbili sawa na kile cha usiku. Kwa jumla mchana na usiku huwa na saa ishirini na nne.

Kipindi hiki cha saa ishirini na nne (siku moja) kinaweza kugawika katika sehemu mbalimbali kama ifuatavyo:

 • Alfajiri mbichi – mwendo kati ya saa tisa na saa kumi na moja asubuhi.
 • Mapambazuko, macheo, mawio - asubuhi jua linapochomoza; mwendo wa saa thenashara asubuhi.
 • Mafungulia ng’ombe – asubuhi mwendo wa saa mbili hadi saa tatu.
 • Adhuhuri – mchana kuanzia saa sita hadi saa tisa.
 • Jua la mtikati – saa sita mchana
 • Jua la utosini –
 • Alasiri – kati ya saa tisa mchana hadi magharibi.
 • Magharibi – wakati jua linapokuchwa/linapotua/linapozama.

 • Machweo/machwa – wakati jua linapozama.
 • Mafungianyama – jioni wakati wanyama wanaporejeshwa kutoka malishoni au machungani.
 • Wakati wa jua kuaga miti – mwendo wa jua kuzama.
 • Jioni – mwendo wa kuanzia alasiri hadi magharibi.
 • Usiku mchanga – kuanzia saa moja hadi saa tano usiku.
 • Usiku wa manane – saa saba hadi saa tisa usiku.
 • Jogoo la kwanza – mwendo wa saa tisa asubuhi.
 • Majogoo – mwendo wa saa kumi na moja asubuhi.

Siku Jumla ya siku saba huwa ni wiki au juma moja.

Siku za wiki ni:

 1. Jumamosi (Sabato),
 2. Jumapili (Dominika),
 3. Jumatatu,
 4. Jumanne,
 5. Jumatano,
 6. Alhamisi,
 7. Ijumaa.

Mpangilio wa siku:

Majuma manne ni sawa na mwezi mmoja. Miezi kumi na miwili ni sawa na mwaka mmoja.

Miezi ya mwaka ni: Januari , Februari, Machi, Aprili, Mei, Juni, Julai, Agosti, Septemba, Oktoba, Novemba, Disemba.

Miaka kumi ni sawa na mwongo.

Kipindi cha miaka mia moja ni sawa na karne.

Kipindi cha miaka elfu moja huitwa kikwi au milenia.